Katibu Tawala wa Mkoa wa Shinyanga, CP Salum Hamduni, leo Oktoba 2, 2025, amepokea rasmi timu ya Mama Samia Legal kikosi maalum cha wataalamu wa sheria kilichofika mkoani Shinyanga kwa ajili ya kutoa msaada wa kisheria katika magereza, hususan kwa wahitaji wasiokuwa na uwezo wa kupata uwakilishi wa kisheria.
Akizungumza wakati wa kuwapokea, CP Hamduni aliipongeza timu hiyo kwa kazi kubwa wanayoifanya ya kuwafikia wananchi walioko magerezani, akisisitiza kuwa serikali ya mkoa iko tayari kutoa ushirikiano wa karibu kuhakikisha huduma hiyo inatolewa kikamilifu na kwa ufanisi.

“Niwakaribishe katika Mkoa wa Shinyanga. Hii ni kazi ya huruma na haki. Tunawapongeza kwa uamuzi wa kuwatumikia wale ambao mara nyingi sauti zao hazisikiki. Serikali ya mkoa ipo pamoja nanyi,” alisema CP Hamduni.
Kwa upande wake, Mratibu wa Mama Samia Legal, Bw. Haruna Matata, alisema kuwa timu hiyo inajumuisha wataalamu kutoka taasisi mbalimbali za serikali ikiwemo Wizara ya Katiba na Sheria, Wizara ya Mambo ya Ndani, Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, pamoja na Makao Makuu ya Magereza.
Bwana Matata alieleza kuwa lengo kuu la programu hiyo ni kusogeza huduma za kisheria karibu na wananchi walio magerezani, hasa wale waliokosa msaada wa uwakilishi wakati wa mashauri yao. Alibainisha kuwa Shinyanga ni mkoa wa pili kutembelewa baada ya Mwanza, katika kampeni ya kitaifa inayolenga kufikia magereza yote 128 nchini.
“Wapo wafungwa wengi waliokosa wanasheria wakati wa kesi zao, na huenda waliadhibiwa bila msaada sahihi wa kisheria. Sisi kama timu ya Mama Samia Legal, tumejipanga kuwapa msaada huo kwa weledi na huruma,” alisema
Huduma hii ni sehemu ya dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha haki inatolewa kwa wote, bila kujali uwezo wa mtu. Zoezi hilo litakuwa endelevu na linaweka historia mpya ya usawa mbele ya sheria kwa watanzania wote.
OFISI YA MKUU WA MKOA, MKOA WA SHINYANGA, 04 MTAA WA BOMA
Anuani: P.O.Box 320, 37180,SHINYANGA, TANZANIA
Simu: +255 28 2762222
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@shinyanga.go.tz
Hakimiliki@2018. Mkoa wa Shinyanga. Haki zote zimehifadhiwa