Katibu Tawala wa Mkoa wa Shinyanga, CP. Salum Hamduni, leo Octoba 6,2025 amepokea rasmi ujumbe wa wataalamu wa afya 25 kutoka Mkoa wa Iringa waliowasili kwa ziara ya mafunzo ya siku mbili, yenye lengo la kujifunza masuala ya usafi wa mazingira, udhibiti wa taka ngumu na usimamizi wa sheria kwenye huduma za afya.
Ujumbe huo unaojumuisha Mganga Mkuu wa Mkoa wa Iringa, waganga wakuu wa wilaya, pamoja na maafisa afya na mazingira, uko mkoani Shinyanga kwa lengo la kubadilishana uzoefu na kujifunza mbinu bora zinazotekelezwa na Mkoa wa Shinyanga katika kuhakikisha mazingira safi, salama na rafiki kwa afya ya binadamu.

Kwa upande wake, Mratibu wa ziara hiyo, Bi. Khadija Haruna, amesema wamevutiwa na mafanikio ya Mkoa wa Shinyanga katika maeneo ya udhibiti wa taka ngumu, usimamizi wa majitaka, ukusanyaji wa mapato kwenye huduma za afya mazingira, pamoja na utekelezaji wa sheria na taratibu zinazolenga kulinda afya ya jamii.
“Shinyanga imekuwa mfano wa kuigwa kwa namna inavyosimamia usafi wa mazingira, hasa kwenye masuala ya taka zinazotokana na huduma za afya. Tumekuja kujifunza ili kwenda kuboresha mifumo yetu Iringa,” amesema Bi. Khadija.
Katika salamu zake za ukaribisho, RAS Hamduni amewapongeza wataalamu hao kwa kuchagua Shinyanga kuwa sehemu ya kujifunzia, na kuahidi kutoa ushirikiano wote kwa kipindi chote watakachokuwa mkoani humo.
Amesisitiza kuwa mkoa unaendelea kuwekeza katika afya ya mazingira kwa kuhakikisha sheria zinasimamiwa kikamilifu na utoaji wa elimu kwa jamii unaimarishwa.

OFISI YA MKUU WA MKOA, MKOA WA SHINYANGA, 04 MTAA WA BOMA
Anuani: P.O.Box 320, 37180,SHINYANGA, TANZANIA
Simu: +255 28 2762222
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@shinyanga.go.tz
Hakimiliki@2018. Mkoa wa Shinyanga. Haki zote zimehifadhiwa