Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Zainab Telack amewataka wanawake Mkoani hapa kuendelea kukaa mkao wa kiume kwenye pikipiki zinazotoa huduma ya usafiri maarufu kama bodaboda.
Mhe. Telacka ameagiza hivyo wakati wa mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye viwanja vya Zimamoto mjini hapa jana kwa lengo la kusikiliza kero mbalimbali za wananchi wa Manispaa ya Shinyanga, ambapo moja ya kero iliyoibuliwa ni baadhi ya wanawake kulalamika kuwa mtindo wa kukaa kwenye pikipiki alioamuru Mkuu wa Mkoa miezi kadhaa iliyopita unawadhalilisha.
Mhe. Telack amesema agizo hilo halina nia ya kuwakomoa wanawake bali ni kuokoa maisha yao kwani mtindo huo wa ukaaji unamfanya mwendesha bodaboda kuendesha vizuri zaidi kuliko wakikaa upande mmoja.
Amesema hivi sasa Serikali inashughulikia kupatikana kwa daladala za mabasi madogo (hiace) na kuwaomba wafanyabiashara kuanza kutoa huduma ya usafiri katikati ya mji kwa kutumia hata magari aina ya Noah wakati Serikali ikiendelea na mchakato huo.
“Najua kinamama hawapendi kukaa kiume, ila kwa sasa tuvumiliane kwani ukipata kilema tayari unashindwa kufanya kazi“amesema Mhe. Telack.
Mkuu wa Mkoa amesema atoe agizo la wanawake kukaa mtindo wa kiume kwenye bodaboda, ajali za bodaboda zimepungua zaidi ya nusu katika Manispaa ya Shinyanga, hivyo amesisitiza wanawake waendelee kukaa mtindo huo ili waepukane ajali zisizo za lazima.
Wakati huo huo, Mhe. Zainab Telack amemulekeza Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga kutoa mafunzo kwa waendesha baiskeli na pikipiki wanaotoa huduma ya usafiri Mjini Shinyanga kwa lengo la kuwapa elimu ya matumizi ya mzunguko (round about) kwani wengi wao hawafahamu namna ya kupita kwenye mzunguko hivyo kusababisha ajali.
Amesema nia ya mafunzo hayo ni kuhakikisha ajali zinapungua na wanakuwa salama.
Boma Street, Mwanza Road
Anuani: P.O.Box 320, Shinyanga
Simu: +255 28 2762222
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@shinyanga.go.tz
Hakimiliki@2018. Mkoa wa Shinyanga. Haki zote zimehifadhiwa