MKUU wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Anamringi Macha leo tarehe 7 Februari, 2025 amefungua Bonanza na michezo ya Jeshi la Wananchi Bezi ya Shinyanga la kuaga mwaka 2024 na kukaribisha mwaka 2025.
Pamoja na mambo mengine RC Macha ameipongeza Bezi ya Shinyanga inayoongozwa na Kanali Raphael Faustine Chachankwa kazi nzuri wanayoifanya sanjari na kuandaa michezo hiyo ambayo imewakutanisha askari wa vikosi vyote hapa Shinyanga na kushiriki michezo mbalimbali ikiwemo mpira wa miguu kati ya Kikosi cha 941 Regt kilichoungana na 976 Regt dhidi ya Kikosi cha 82 Regt kilichoungana na 516 KJ.
RC Macha amefungua bonanza hilo katika viwanja vya Fresho vilivyopo Manispaa ya Shinyanga na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Katibu Tawala Mkoa wa Shinyanga CP. Salum Hamduni, Mkuu wa Bezi ya Shinyanga Kanali Raphael Faustine Chacha na Maafisa wengine kutoka Bezi ya Shinyanga na kusisitiza kuwa Wanashinyanga na Watanzania kwa ujumla wanajivunia sana uwepo wa jeshi hili la wananchi.
"Pamoja na bonanza hili zuri la michezo, lakini pia ninawapongeza sana kwa kazi nzuri mnayoifanya, tunayo amani ya kutosha na utulivu mkubwa nchini kwetu, hakika kwakweli tunajivunia sana uwepo wenu," amesema RC Macha.
Awali akitoa taarifa kwa mgeni rasmi, Kanali Raphael alisema Bezi ya Shinyanga ilianza kwa kutembelea na kutoa misaada mbalimbali ya kiutu kwa Kituo cha kulea Watoto Yatima cha Lohada kilichopo Kata ya Kitangili Manispaa ya Shinyanga huku akisisitiza kuwa Jeshi la Wananchi Bezi ya Shinyanga litaendelea kuandaa bonanza kama hizo kila wakati na kwamba wataendela kumuomba ili aendelee kushiriki nao kila itakapohitajika.
Huu ni utaratibu wa kawaida wa Jeshi la Wananchi Bezi ya Shinyanga wa kuandaa na kushiriki katika Bonanza mbalimbali kwa lengo la kuwakutanisha ili kushiriki michezo mseto ukiachilia mbali hili la leo ambalo lilikuwa maalum kwa lengo la kuaga mwaka 2024 na kukaribisha mwaka 2025.
Boma Street, Mwanza Road
Anuani: P.O.Box 320, Shinyanga
Simu: +255 28 2762222
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@shinyanga.go.tz
Hakimiliki@2018. Mkoa wa Shinyanga. Haki zote zimehifadhiwa