Na. Paul Kasembo, SHY RS.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Anamringi Macha leo Machi 25, 2025 amekutana na kufanya mazungumzo na Uongozi wa Shirika la Standing Voice linalojishughulisha na utoaji wa huduma kwa watu wenye Ualbino ambao wanafanya kiliniki za uchunguzi wa ngozi na macho katika Hospitali za Wilaya mkoani Shinyanga, Shule zenye wanafunzi wenye ualbino pamoja na makao za watoto zenye watoto wenye ualbino
RC Macha pamoja na mambo mengine amewashukuru na kuwapongeza Shirika la Standing Voice kwa kuendelea kushirikiana na Serikali kupitia Maafisa Ustawi wa Jamii ili kuwatunza watoto wenye Ualbino kuwalinda dhidi ya ukatili lakini pia amewahakikishia kuwa uongozi wa Mkoa uko tayari wakati wote kushirikiana nao bega kwa bega wanapotimiza majukumu yao.
“Ninawapongeza kwa kazi nzuri mnayoifanya ya kuwatunza na kuwalinda watoto wenye ualbino dhidi ya hatari za ukatili lakini pia na huduma ya matibabu lakini niwahakikishie kuwa uongozi wa Mkoa kupitia Maafisa Ustawi wa Jamii unawakaribisha sana na upo tayari kushirikiana nanyi bega kwa bega mnapotimiza majukumu yenu” amesema RC Macha.
Kwa upande wake Mratibu wa Afya kutoka Shirika la Standing Voice Bi. Christina Silas, ameeleza kuwa wamekuwa wakifanya Kliniki ya ngozi kwa watu wenye ualbino kila baada ya miezi sita (6) kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa na Ofisi za Wakurugenzi wa Halmashauri kupitia Maafisa Ustawi wa Jamii pamoja na madaktari kutoka Hospitali ya Kilimanjaro Christian Medical Centre (KCMC).
Shirika la Standing Voice linajishughulisha na utoaji wa huduma za Kliniki ya ngozi kwa watu wenye ualbino ili kufanyiwa uchunguzi wa ngozi na macho, utoaji wa elimu mbalimbali pamoja na mahitaji mengine kwa watu wenye ualbino yakiwemo kutoa kofia pana za kujikinga na mionzi ya jua, mafuta maalumu pamoja na miamvuli na endapo mtu atabainika kuwa na dalili za kansa hupewa rufaa kwenda Hospitali ya Kanda ya Bugando au Hospitali ya Ocean Road na Shirika hugharamia matibabu hayo.
Boma Street, Mwanza Road
Anuani: P.O.Box 320, Shinyanga
Simu: +255 28 2762222
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@shinyanga.go.tz
Hakimiliki@2018. Mkoa wa Shinyanga. Haki zote zimehifadhiwa