Na.Paul Kasembo, KAHAMA.
MKUU wa Mkoa wa Shinyanga Mhe.Anamringi Macha amepokea Nyaraka kutoka kwa Katibu wa Chama Cha Mapinduzi Taifa Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi zilizobeba kero za wananchi wa Wilaya ya Kahama na kuahidi kuzifanyia kazi huku akiwaomba kuwa watulivu wakisubiri kero zao zitatuliwe.
RC Macha ameyasema haya leo tarehe 10 Oktoba, 2024 baada Balozi Dkt. Nchimbi kupokea kero kutoka kwa wananchi akiwa katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika viwanja vya Majengo na ambao ulilenga kupokea, kusikiliza na kutatua kero zao ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Ilani ya CCM.
“Nimepokea Nyaraka hizi zilizobeba kero za Wanakahama kutoka kwa Balozi Dkt. Nchimbi na mimi naahidi kuanza kuzifanyia kazi punde baada ya ziara hii kukamilika ili kuhakikisha zinatatuliwa ndani ya muda mfupi, lakini niwaombe Wanakahama muendelee kuwa watulivu kwa kipindi hiki mnachosubiria kero hizi kupatiwa ufumbuzi” amesema RC Macha.
Kando na hilo, suala la uhaba wa umeme liliwasilishwa na Waheshimiwa Wabunge wa Wilaya ya Kahama ambapo wameomba na kupendekeza Wilaya ya Kahama kufanywa kuwa Mkoa wa Ki - TANESCO ili kupunguza changamoto ya umeme.
Kufuatia ombi hili, Dkt. Nchimbi amewasiliana na Naibu Waziri Mkuu ambaye pia ni Waziri wa Nishati Mhe. Dotto Biteko ambaye alisema kuwa ameshapokea mapendekezo hayo na sasa anayafanyia kazi ili kuhakikisha Wilaya ya Kahama inakuwa Mkoa wa Kitanesko.
Hii ni siku ya pili ya ziara ya Balozi Dkt. Nchimbi hapa mkoani Shinyanga, ambapo kesho atahitimisha hapa wilayani Kahama na baadae atafanya mkutano wa hadhara Manispaa ya Shinyanga kisha Kata ya Maganzo iliyopo wilayani Kishapu.
Boma Street, Mwanza Road
Anuani: P.O.Box 320, Shinyanga
Simu: +255 28 2762222
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@shinyanga.go.tz
Hakimiliki@2018. Mkoa wa Shinyanga. Haki zote zimehifadhiwa