RC MACHA APONGEZA UJENZI WA HOSPITALI YA WILAYA YA MSALALA
Na. Paul Kasembo, Msalala.
MKUU wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Anamringi Macha amepongeza ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Msalala yenye majengo 15 ambayo imeanza kutoa huduma za afya mwezi Oktoba, 2022 huku akiwataka kuanzisha utaratibu wa kufanya vipimo kwa wananchi ambao siyo wagonjwa hasa wazee ili waweze kujuwa afya zao ikiwemo kipiko cha Figo.
RC Macha amemshukuru sana Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuwezesha fedha za ujenzi wa Hospitali hii na kuwataka watumishi wa afya kuwa na lugha nzuri, uzalendo na uchapakazi ili kuunga mkono juhudi za Mhe. Rais.
Macha ameyasema haya leo tarehe 20 Mei, 2024 mara baada ya kukagua majengo, kuongea na wagonjwa pamoja na kupokea taarifa ya ujenzi huu ambao umejumuisha na nyumba za wahudumu wa Hospitali wakiwemo Madaktari ili kuwa karibu na utoaji huduma.
"Nimeridhishwa na ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Msalala, hakika nawapongeza sana kwa mradi huu na kwakweli mmenifariji sana na kunifurahisha kulinganisha na baadhi ya eneo niliyopita kukagua Sekta hii ya afya, Msalala nawapongeza sana hongereni sana na pia tuendelee kumshukuru sana Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwezesha ujenzi huu," amesema RC Macha.
Pamoja na mambo mengine, pia ameitaka TARURA Wilaya ya Kahama kuangalia namna ya kutengeneza barabara inayoingia Hospitalini hapo ili iweze kupitika wakati wote na bila kuwa shida ukizingatia inapeleka na kutoa wagonjwa wetu.
Akisoma taarifa ya Hospitali, Daktari Samweli Mapula ambaye ni Mganga Mfawidhi Hospitali ya Wilaya ya Msalala amesema kuwa mpaka sasa zaidi ya Bil. 2 zimekwisha kutumika katika ujenzi huu ulioanza mwaka 2019 na inahudumia wananchi katika Kata 18 za Halmashauri ya Wilaya ya Msalala pamoja na Halmashauri jirani za Mkoa wa Geita (Mbogwe).
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Msalala Ndg. Khamis Katimba amemueleza RC Macha kuwa yale yote aliyoelekeza na kushauri wameyapokea na kwamba watayafanyia kazi kwa haraka na kwa weledi zaidi ili kuboresha huduma kwa wananchi.
HABARI PICHA
Boma Street, Mwanza Road
Anuani: P.O.Box 320, Shinyanga
Simu: +255 28 2762222
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@shinyanga.go.tz
Hakimiliki@2018. Mkoa wa Shinyanga. Haki zote zimehifadhiwa