Na. Paul Kasembo, SHY RS.
MKUU wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Anamringi Macha ametoa wito wa kuwataka wazazi na walezi wote Mkoani Shinyanga kuhakikisha wanashiriki kikamilifu katika kuhamasisha, kuwaruhusu au kuwapeleka wasichan wenye umri wa kati ya miaka 9 hadi 14 katika shule zilizokaribu nao kwa ajili ya kupatiwa chanjo muhimu dhidi ya Saratani ya mlango wa kizazi huku akisisitiza kuwa chanjo hii haina madhara yoyote wa watoto wa kike.
Haya yamesemwa leo tarehe 22 Aprili, 2024 kwenye hafla yenye sura ya Kimkoa katika viwanja vya Shule ya Msingi Ndala A iliyopo Kata ya Masekelo, Manispaa ya Shinyanga ambapo RC Macha alikuwa akizindua Kampeni ya Wiki ya Chanjo ambayo imeanza leo na itadumu hadi tarehe 28, Aprili 2024 na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Kiserikali, Kisiasa, wananchi na walengwa wenyewe ambao ni wanafunzi.
"Natoa wito huu kwenu wazazi na walezi wote Mkoa wa Shinyanga mhakikishe kuwa mnahamasisha na kuwapeleka watoto wenu wenye umri wa kati ya miaka 9 hadi 14 wakapate chanjo ukizingatia kuwa chanjo hii haina madhara yoyote," amesema RC Macha.
RC Macha amewakumbusha wananchi wote kuwa, kujuwa afya zao ni muhimu sana, hivyo kila mwananchi ajiwekee utaratibu wa kuwa anapima mara kwa mara hata kama haugui ili kuweza kujuwa mwenendo wa mwili wake badala ya kusubiria tukio muhimu kama hili.
Kando na hayo RC Macha pia ametoa angalizo kwa yeyote atakayejaribu kutumia mitandao ya kijamii kundika au kuripoti taarifa zinazohusu chanjo hii kwa lengo la kupotosha umma kwamba atachukuliwa hatua kali za kisheria ikiwa ni pamoja na kupelekwa mahakamani, kama hajaelewa ni vema akaja kupata ufafanuzi kwa wataalam wetu ambao watakuwa wakipatikana katika shule zote.
Chanjo hii iliyoanza kutolewa rasmi hapa Shinyanga, inatarajia kuwanufaisha wasichana 198,865 katika shule 887 ambapo kutakuwa na vituo vya kutolea huduma 238 na jumla ya Timu ya watoa huduma itakayohusika ni 242 na lengo litafikiwa kwa asilimia 100.
HABARI PICHA
RC Macha (kushoto) akimpatia zawadi mtoto wa kwanza kupata chanjo
Mkuu wa Wilaya ya Kishapu Mhe. Joseph Mkude ambaye anakaimu Wilaya ya Shinyanga akielezea jambo wakati wa uzinduzi
Mganga Mkuu Mkoa wa Shinyanga Daktari Yudas Ndungile
Boma Street, Mwanza Road
Anuani: P.O.Box 320, Shinyanga
Simu: +255 28 2762222
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@shinyanga.go.tz
Hakimiliki@2018. Mkoa wa Shinyanga. Haki zote zimehifadhiwa