Na. Paul Kasembo, SHY RS.
MKUU wa Mkoa wa Shonyanga Mhe. Anamringi Macha amewaomba viongozi wa dini zote kuendelea kutoa mafundisho yaliyo sahihi kwa waumini ambao ndiyo wananchi kwa upande wa Serikali ili kuweza kuleta maslahi mapana kwa pande zote mbili pamoja na kusaidia utoaji wa elimu katika nyanja mbalimbali kwa umma huku akisisitiza kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na Madhehebu yote ya dini katika kufikia lengo na maono ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuwawezesha wananchi kuishi kwa amani na kuinua maisha yao kiuchumi, kijamii na kiutamaduni katika maeneo yao.
RC Macha ameyamesema haya leo tarehe 26 Mei, 2024 alipokuwa akihutubia waumini wa Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT) yenye wanachama 14 kutoka Madhehebu ya Kiprotestanti yenye mwelekeo wa Kikanisa kutoka Tanzania Bara na Visiwani ambayo ilianzoshwa tarehe 23 Jan, 1934 ambapo leo inatimiza miaka 90 ya uwepo wake ikiwa leo ni MAADHIMISHO YA SIKU YA CCT huku maadhimisho yakianisha baadhi ya lengo kuwa ni Kuimarisha Uinjilisti kikamilifu unaozingatia mafundisho yenye msingi wa YESU KRISTO.
"Niwaombe sana Viongozi wote wa Dini kuendelea kutoa mafundisho yaliyo sahihi kwa waumini ambao ndiyo wananchi kwa upande wa Serikali kuweza kuleta maslahi mapana kwa pande zote mbili pamoja sanjari na kutoa elimu kwa umma lengo ni kufikia kusudio kwa wananchi," amesema RC Macha.
Kando na wito huo, pia amewataka viongozi wa dini Mkoani Shinyanga kuendelea kutoa elimu ya utunzaji wa mazingira, kuimarisha usafi na kuelekeza jitihada katika kuelimisha waumini na wananchi juu ya matumizi ya Nishati Safi huku akisisitiza kwamba Serikali itaendelea kuweka miundombinu ya mazingira rafiki na wezeshi ili kuimarisha matumizi haya ya nishati safi ukizingatia Mkoa wa Shinyanga moja ya kazi kuu ni uchimbaji wa madini.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Mhe. Julius Mtatiro ametumia nafasi hii kuwakumbusha waumini wa CCT dhima ya Uumbaji na kwa nini tupo hapa duniani huku akisisitiza kupendana na kusaidiana wakati wote na huu ndiyo wito wake kwa waumini wote.
Boma Street, Mwanza Road
Anuani: P.O.Box 320, Shinyanga
Simu: +255 28 2762222
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@shinyanga.go.tz
Hakimiliki@2018. Mkoa wa Shinyanga. Haki zote zimehifadhiwa