Na. Paul Kasembo, SHY RS.
MKUU wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Anamringi Macha amewataka wajumbe wa Bodi ya Maji Bonde la Kati kufanya uchaguzi wa viongozi wao kwa umakini, uangalifu na uaminifu zaidi huku akisisitiza ushiriki wa wadau uwe madhubuti kwa kila mdau na kuhakikisha habaki nyuma katika kila zoezi litakalofanyika katika kikao hiki.
Mhe. Macha ameyasema haya leo tarehe 7 Agosti, 2024 alipokuwa akifungua kikao hiki cha wajumbe wa Bodi ambapo pamoja na mambo mengine pia amewataka wajumbe kubainisha na kujadili changamoto mbalimbali zilizopo katika kidakio cha maji Sibiti sanjari na kushirikiana kuhusu shughuli za usimamizi wa rasilimali za maji.
"Niwaagize wajumbe wa Bodi ya Maji ya Bonde la Kati kuhakikisha mnafanya uchaguzi wa viongozi wenu kwa umakini, uaminifu na uangalifu mkubwa ili lengo la Serikali na Ilani ya Chama Cha Mapinduzi la kuhakikisha wananchi wanasogezewa huduma ya maji inafikiwa walau kwa asilimia 95 mijini na 85 vijijini ifikapo mwaka 2025 kama ilivuoahidiwa," amesema RC Macha.
Aidha RC Macha amesema kuwa, falsafa ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha anamtua ndoo mama kichwani inakwenda vizuri sana ambapo mpaka sasa Mkoa wa Shinyanga umepewa fedha zaidi ya Bil. 77 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maji, yote inalenga utekelezaji wa maono ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Awali ndg. Julius Kagoma ambaye ni Kaimu Mkurugenzi Bodi ya Maji Bonde la Kati alimueleza mgeni rasmi pamoja na wajumbe kuwa pamoja na mambo mengine wamekutana katika kikao cha Uundaji wa Kamati ya Kidaka Maji cha Sibiti (Sibiti Catchment Committee) ili kufanya uchaguzi wa viongozi pamoja na kuandaa mpango kazi utakaotumika kuongoza utendaji kazi wa Bodi itakayoundwa.
Kwa ujumla Bodi ya Maji Bonde la Kati iliyoundwa chini ya kifungu cha 22 cha Sheria ya Usimamizi wa Rasilimali za Maji Na.11 ya mwaka 2009 na marekebisho yake Na. 8 ya mwaka 2022 inajukumu kuu la kusimamia rasilimali za maji ikiwemo utunzaji na uhifadhi wa vyanzo vya maji.
Boma Street, Mwanza Road
Anuani: P.O.Box 320, Shinyanga
Simu: +255 28 2762222
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@shinyanga.go.tz
Hakimiliki@2018. Mkoa wa Shinyanga. Haki zote zimehifadhiwa