Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Mboni Mhita, amekutana na kufanya mazungumzo na Bi. Furaha Comoro, ambaye ni Mratibu mpya wa Mahusiano ya Jamii wa Mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP) katika Mkoa wa Shinyanga.
Bi. Furaha Comoro ametambulishwa rasmi leo tarehe 8 Septemba, 2025 kwa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga akichukua nafasi ya Bi. Cecilia Nzeganije ambaye amehamishiwa Mkoa wa Geita. Katika kikao hicho kifupi kilichofanyika ofisini kwa Mkuu wa Mkoa, Bi. Cecilia alitoa shukurani kwa ushirikiano alioupata kutoka kwa viongozi wa Serikali mkoani humo katika kipindi chote cha utumishi wake.
Kwa upande wake, Bi. Furaha Comoro alieleza dhamira yake ya kuendeleza ushirikiano mzuri uliopo baina ya EACOP na uongozi wa Mkoa wa Shinyanga, hasa katika kuhakikisha wananchi wananufaika kwa usawa na kwa haki na fursa mbalimbali zitokanazo na mradi huo mkubwa wa kimkakati.
Mkuu wa Mkoa, Mhe. Mhita, alisisitiza umuhimu wa kuendeleza misingi ya uwazi, ushirikiano wa karibu na mawasiliano ya mara kwa mara baina ya Serikali na wadau wa mradi huo, akibainisha kuwa Serikali ya Mkoa itaendelea kutoa ushirikiano kuhakikisha mradi unatekelezwa kwa mafanikio na kwa kuzingatia maslahi ya wananchi.
OFISI YA MKUU WA MKOA, MKOA WA SHINYANGA, 04 MTAA WA BOMA
Anuani: P.O.Box 320, 37180,SHINYANGA, TANZANIA
Simu: +255 28 2762222
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@shinyanga.go.tz
Hakimiliki@2018. Mkoa wa Shinyanga. Haki zote zimehifadhiwa