Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Mboni Mhita, leo Agosti 19,2025 amekutana na Naibu Waziri wa Madini Mhe. Dkt. Steven Kiruswa pamoja na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe. Daniel Sillo, katika kikao kazi kilichofanyika ofisini kwake kwa lengo la kujadili mwenendo wa shughuli za uokoaji kufuatia ajali ya kuporomoka kwa Mgodi wa Nyandolwa uliopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga.
Katika mazungumzo hayo, RC Mhita ameeleza kuwa Serikali ya Mkoa kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama, taasisi za uokoaji pamoja na wadau mbalimbali, inaendelea na jitihada za kuwaokoa wachimbaji waliokwama mgodini tangu kutokea kwa ajali hiyo.
Mhe. Mhita amethibitisha kuwa hadi sasa jumla ya watu wanane (8) wameopolewa kutoka mgodini, ambapo kwa masikitiko makubwa mwili wa fundi mwingine umepatikana akiwa amefariki dunia, na hivyo kufanya idadi ya waliofariki kufikia watano. Aidha, mafundi 17 bado hawajafikiwa, na juhudi za kuwatafuta zinaendelea kwa kasi na umakini mkubwa.
“Tunafanya kazi usiku na mchana kuhakikisha tunawafikia wote waliokwama. Serikali imeweka nguvu kubwa katika eneo hili la uokoaji, na tunashukuru kwa ushirikiano kutoka kwa vyombo vyote husika,” alisema Mhita.
RC Mhita pia amepongeza ujio wa Manaibu Waziri hao kwa kuonesha mshikamano na uzito wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kushughulikia maafa ya aina hii, huku akiendelea kuwapa pole ndugu na familia za waathirika wa tukio hilo.
Serikali ya Mkoa imeendelea pia kutoa msaada wa chakula kwa familia zilizoathirika, na kuimarisha huduma muhimu katika eneo la tukio ili kuleta faraja kwa ndugu wanaosubiri hatima ya wapendwa wao.
Boma Street, Mwanza Road
Anuani: P.O.Box 320, Shinyanga
Simu: +255 28 2762222
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@shinyanga.go.tz
Hakimiliki@2018. Mkoa wa Shinyanga. Haki zote zimehifadhiwa