Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Mboni Mhita, @mboni_mhita leo Septemba 26, 2025, ametembelea Kijiji cha Isela kilichopo katika Manispaa ya Shinyanga, kwa lengo la kutoa pole kwa familia zilizopatwa na msiba kufuatia ajali ya gari iliyogonga pikipiki na kusababisha kifo cha mtu mmoja na majeruhi mmoja.
Katika ziara hiyo, Mhe. Mhita ameagiza Wakala wa Barabara (TANROADS) Mkoa wa Shinyanga kuhakikisha wanajenga matuta na kuweka taa za barabarani katika eneo hilo ili kupunguza kasi ya magari na kuongeza usalama kwa watumiaji wa barabara, hususan waendesha pikipiki na waenda kwa miguu.
“Nimesikitishwa na ajali hii, lakini tunapaswa kuchukua hatua madhubuti kuhakikisha tunazuia ajali zinazoweza kuepukika. TANROADS naomba mara moja waanze utekelezaji wa ujenzi wa matuta na taa katika eneo hili,” amesema Mhita.
Kwa upande wake, Muhandisi Fred Kipamila Kaimu Meneja TANROADS mkoani hapa ameahidi kutekeleza agizo hilo kwa haraka, akieleza kuwa taratibu za awali zimeanza kuchukuliwa ili kuhakikisha usalama wa wananchi unaimarika.
Aidha, Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Wakili Julius Mtatiro @julius_mtatiro aliwataka wananchi kuepuka matumizi ya vileo barabarani na kuzingatia sheria za usalama, akisisitiza waendesha bodaboda kuhakikisha pikipiki zao zina vifaa vya usalama ikiwemo vioo vya pembeni (side mirrors).
Nao wananchi wa Isela wameishukuru Serikali kwa hatua hiyo, wakisema imekuwa ni kilio chao cha muda mrefu kutokana na ajali za mara kwa mara zinazotokea katika eneo hilo.
Ziara hiyo ni sehemu ya jitihada za Serikali ya Mkoa wa Shinyanga kuhakikisha maisha ya wananchi yanalindwa kwa kuweka mazingira salama, hasa katika maeneo yenye changamoto za miundombinu.
OFISI YA MKUU WA MKOA, MKOA WA SHINYANGA, 04 MTAA WA BOMA
Anuani: P.O.Box 37180,SHINYANGA, TANZANIA
Simu: +255 28 2762222
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@shinyanga.go.tz
Hakimiliki@2018. Mkoa wa Shinyanga. Haki zote zimehifadhiwa