Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Mboni Mhita amepokea kombe la ushindi wa mashindano ya SHIMISEMITA kutoka kwa Timu ya Mpira wa Miguu ya Halmashauri ya Wilaya ya Msalala, ambayo imeibuka bingwa wa mwaka huu baada ya kuifunga Geita DC kwa mikwaju ya penalti 4-2 katika mchezo wa fainali uliofanyika kwenye Uwanja wa Mkwakwani, Jijini Tanga.

Akizungumza leo Septemba 19, 2025 wakati wa hafla ya mapokezi ya kombe hilo iliyofanyika kwenye ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Manispaa ya Shinyanga, Mhe. Mhita ameipongeza timu ya Msalala kwa kuonesha uwezo mkubwa na kuutangaza Mkoa wa Shinyanga katika mashindano hayo ya watumishi wa serikali kutoka halmashauri mbalimbali nchini.
“Tuna kila sababu ya kujivunia mafanikio haya. Ushindi huu ni ishara ya juhudi, nidhamu na mshikamano wa watumishi wetu. Nawapongeza sana Msalala kwa kutuwakilisha vyema na kurudi na heshima hii,” amesema RC Mhita.

Katika hatua nyingine, RC Mhita ameziagiza halmashauri zote mkoani Shinyanga kutenga maeneo maalum ya michezo kwa ajili ya watumishi ili kuendeleza vipaji na kujenga afya kupitia ushiriki wa mashindano mbalimbali kama SHIMISEMITA, SHIMIWI.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Msalala, Bi. Rose Manumba, amesema ushindi huo ni matokeo ya maandalizi ya muda mrefu, mshikamano wa timu na sapoti kutoka kwa uongozi.
Amesema kuwa ushindi huo umeongeza ari ya kujiandaa kikamilifu kwa mashindano yajayo kwa lengo la kuutangaza vema mkoa wa Shinyanga na Halmashauri ya Msalala kitaifa.
“Tutaendelea kuwekeza katika maandalizi ya timu na kutoa motisha kwa wachezaji ili tuendelee kuleta heshima kubwa zaidi kwa mkoa wetu,” amesema Manumba.

OFISI YA MKUU WA MKOA, MKOA WA SHINYANGA, 04 MTAA WA BOMA
Anuani: P.O.Box 320, 37180,SHINYANGA, TANZANIA
Simu: +255 28 2762222
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@shinyanga.go.tz
Hakimiliki@2018. Mkoa wa Shinyanga. Haki zote zimehifadhiwa