Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Mboni Mhita @mboni_mhita Septemba 26, 2025, alifanya ziara katika Shule ya Sekondari ya Wasichana Shinyanga kwa lengo la kujionea maendeleo ya shule hiyo pamoja na kuzungumza moja kwa moja na walimu na wanafunzi.
Katika ziara hiyo, Mhe. Mhita alipata fursa ya kutembelea miundombinu ya shule hiyo, ikiwa ni pamoja na madarasa, mabweni, maktaba na maeneo ya kujifunzia ili kubaini changamoto zinazowakabili wanafunzi na walimu, na kuona namna ya kuzitatua kwa kushirikiana na wadau wa elimu.
Akizungumza na wanafunzi wa shule hiyo, RC Mhita aliwahimiza kusoma kwa bidii, kuwa na nidhamu na kutambua nafasi yao muhimu kama viongozi wa kesho. Alisisitiza kuwa Serikali inatambua umuhimu wa kumwezesha mtoto wa kike kwa kumpatia mazingira rafiki ya kujifunzia na kujilea.
“Ninyi wasichana mna nafasi kubwa katika maendeleo ya jamii yetu. Elimu ndiyo silaha yenu ya kupambana na changamoto za maisha. Jitahidini, msome kwa bidii, na mjitunze,” alisema Mhe. Mhita.
Kwa upande wa walimu, aliwapongeza kwa kazi kubwa wanayoifanya ya kulea na kuelimisha watoto wa kike huku akiwaasa kuendelea kuwa walezi bora na mifano ya kuigwa katika jamii.
Ziara hiyo pia ilihusisha mazungumzo ya ana kwa ana kati ya Mkuu wa Mkoa na uongozi wa shule, ambapo walimu walieleza mafanikio na changamoto mbalimbali ikiwemo Samani na uhaba wa vifaa vya kufundishia, kama vile Vitabu vya kiada na ziada na Vifaa vya Kompyuta.
Mhe. Mhita alihitimisha kwa kusema kuwa Serikali ya Mkoa itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kuhakikisha kuwa elimu kwa mtoto wa kike inabaki kuwa kipaumbele, ili kuleta usawa wa kijinsia na kuendeleza maendeleo ya taifa.
OFISI YA MKUU WA MKOA, MKOA WA SHINYANGA, 04 MTAA WA BOMA
Anuani: P.O.Box 37180,SHINYANGA, TANZANIA
Simu: +255 28 2762222
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@shinyanga.go.tz
Hakimiliki@2018. Mkoa wa Shinyanga. Haki zote zimehifadhiwa