Na Johnson James - Shinyanga RS
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Mboni Mhita, amekutana na kufanya mazungumzo na Wajumbe wa Jumuiya ya Maridhiano na Amani Mkoa wa Shinyanga waliomtembelea ofisini kwake kwa lengo la kumkaribisha rasmi mkoani humo pamoja na kujitambulisha kama wadau wa kudumisha amani na mshikamano katika jamii.
Akizungumza leo Octoba 16,2025 katika kikao hicho, Mhe. Mhita @mboni_mhita ameipongeza jumuiya hiyo kwa kazi kubwa wanayoifanya ya kuhakikisha kunakuwepo na utulivu, mshikamano, uvumilivu wa kidini na kijamii, na kuwaahidi ushirikiano wa karibu katika kufanikisha dhamira ya serikali ya kudumisha amani na maendeleo kwa wote.
“Amani ni msingi wa kila kitu maendeleo, uwekezaji, elimu na hata ustawi wa jamii. Nafurahi sana kuona Kamati hii ipo hai na inaendelea kufanya kazi kwa uzalendo mkubwa. Serikali ipo tayari kushirikiana nanyi bega kwa bega,” alisema Mhita.

Hata Hivyo Mhe. Mhita aliongeza kuwa Ofisi yake itaendelea kushirikiana na kamati hiyo katika kuhakikisha Amani inakuwepo Katika mkoa huo kabla na baada ya Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Octoba 29 Mwaka huu.
Kwa upande wao, Wajumbe wa Kamati hiyo wakiongozwa na Mwenyekiti wao Sheikh Balilusa Khamis wamempongeza Mhe. Mhita kwa kuteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga na kumhakikishia kuwa wapo tayari kuendelea kuwa chombo cha mshikamano, maridhiano na mawasiliano kati ya serikali na jamii, ili kulinda misingi ya amani mkoani humo.
Pia, waliomba Mkuu wa Mkoa kuendelea kuwapa nafasi ya kushirikiana na taasisi nyingine na kutoa elimu kuhusu masuala ya utatuzi wa migogoro, uvumilivu wa kidini, na kukuza maelewano katika maeneo yenye changamoto mbalimbali.

Mkutano huo ni ishara ya mshikamano uliopo baina ya Serikali na wadau wa amani, huku ukisisitiza wajibu wa kila mmoja katika kulinda tunu ya taifa -AMANI.
OFISI YA MKUU WA MKOA, MKOA WA SHINYANGA, 04 MTAA WA BOMA
Anuani: P.O.Box 320, 37180,SHINYANGA, TANZANIA
Simu: +255 28 2762222
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@shinyanga.go.tz
Hakimiliki@2018. Mkoa wa Shinyanga. Haki zote zimehifadhiwa