Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Mboni Mhita @mboni_mhita amempongeza mkandarasi wa ujenzi wa barabara ya Kahama Kakola kwa kazi nzuri na kasi ya utekelezaji wa mradi huo muhimu wa miundombinu, ambao unatajwa kuwa kiunganishi muhimu kati ya Mkoa wa Shinyanga na Geita.
Akizungumza hivi karibuni mara baada ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa barabara hiyo yenye urefu wa kilometa 73.1, pamoja na kambi ya kutengeneza malighafi, Mhita alieleza kuridhishwa na hatua iliyofikiwa hadi sasa – ambapo ujenzi umefikia asilimia 45.16.
“Kasi hii inatia moyo. Barabara hii si tu itarahisisha usafiri kwa wakazi wa Kahama, Msalala na maeneo ya jirani, bali pia ni mhimili wa shughuli za kiuchumi, hasa kwa wadau kama Barick ambao hutumia njia hii kusafirisha mitambo na malighafi kwenda Mgodi wa Bulyanhulu,” alisema Mhita.
Aidha, RC Mhita alisisitiza kuwa Serikali ya Mkoa itaendelea kufuatilia kwa karibu utekelezaji wa mradi huo kuhakikisha unakamilika kwa wakati kama ilivyopangwa.
Kwa upande wake, Meneja wa TANROADS Mkoa wa Shinyanga, Mhandisi Joel Mwambungu, alisema barabara hiyo inajengwa kwa viwango vya kimataifa, ikiwa na upana wa mita 10 hadi 11, huku senta zote zikipangwa kufungwa taa za barabarani kwa ajili ya usalama na uzuri wa miji.
Mradi huu mkubwa wa barabara unatekelezwa kwa gharama ya Shilingi bilioni 106, ukifadhiliwa na kampuni ya Barick kwa kushirikiana na Serikali ya Tanzania. Ujenzi huo unatarajiwa kukamilika rasmi ifikapo Septemba 4, 2026.
Barabara ya Kahama Kakola ikikamilika, itakuwa kichocheo kikubwa cha maendeleo kwa mikoa ya Kanda ya Ziwa na kuinua uchumi wa wananchi kupitia biashara, huduma na usafiri wa uhakika.
OFISI YA MKUU WA MKOA, MKOA WA SHINYANGA, 04 MTAA WA BOMA
Anuani: P.O.Box 320, 37180,SHINYANGA, TANZANIA
Simu: +255 28 2762222
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@shinyanga.go.tz
Hakimiliki@2018. Mkoa wa Shinyanga. Haki zote zimehifadhiwa