Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Mboni Mhita @mboni_mhita amepongeza wahitimu 81 wa Programu Maalum ya Wanawake na Samia kwa kukamilisha mafunzo ya miezi miwili ya kuwajengea uwezo wa kiujuzi na kiuchumi, huku akiahidi kuwa serikali itaendelea kuwaunga mkono kupitia fursa za mikopo na miradi mbalimbali ya kimaendeleo.
Akizungumza leo, Oktoba 2, 2025, katika hafla ya mahafali yaliyofanyika katika Chuo cha VETA Shinyanga, Mhe. Mhita alisema serikali ya Mkoa itaendelea kushirikiana kwa karibu na wanawake waliohitimu ili kuhakikisha wanatumia ujuzi waliopata kujitegemea na kuchangia ustawi wa jamii na taifa kwa ujumla.
“Tuna dhamira ya dhati ya kuwawezesha wanawake. Kupitia programu hii, mmepata msingi mzuri wa ujuzi. Ni jukumu lenu sasa kubadilisha maarifa hayo kuwa fursa halisi za kuboresha maisha yenu,” alisema Mhita.
Alitoa wito kwa wahitimu hao kujiunga na vikundi mbalimbali ili waweze kunufaika na mikopo inayotolewa kupitia halmashauri za mkoa huo, mikopo itakayosaidia kukuza uchumi wao kupitia maarifa waliyopata.
Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Samia, Bi. Futuma Madidi, alitumia fursa hiyo kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, kwa kuona umuhimu wa kuwawezesha wanawake kiuchumi, huku Mkuu wa VETA Mkoa wa Shinyanga, Bw. Abraham Mbughuni, akieleza kuwa wahitimu hao walipatiwa mafunzo ya vitendo katika fani mbalimbali ikiwemo: saluni, ushonaji, mapishi, madereva, umeme, mapambo, kompyuta na ufundi bomba.
Wahitimu walikabidhiwa vyeti na kuhamasishwa kuanzisha vikundi vya uzalishaji na kutumia stadi walizojifunza kujiletea maendeleo.
Katika kuhitimisha hafla hiyo, RC Mhita aliwasihi wananchi wa Shinyanga kujitokeza kwa wingi kushiriki Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba 29, 2025 kwa amani na utulivu. Alisisitiza kuwa Shinyanga itaendelea kuwa ngome ya utulivu na mshikamano, na kwamba wananchi wasiwe na wasiwasi kwani serikali itahakikisha ulinzi na usalama vinakuwepo siku hiyo.
OFISI YA MKUU WA MKOA, MKOA WA SHINYANGA, 04 MTAA WA BOMA
Anuani: P.O.Box 320, 37180,SHINYANGA, TANZANIA
Simu: +255 28 2762222
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@shinyanga.go.tz
Hakimiliki@2018. Mkoa wa Shinyanga. Haki zote zimehifadhiwa