Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Mboni Mhita @mboni_mhita amefanya ziara ya ukaguzi katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga , ambapo amepongeza juhudi za uongozi na watumishi wa hospitali hiyo kwa utoaji mzuri wa huduma kwa wananchi.
Katika ziara hiyo, RC Mhita alipata fursa ya kutembelea wodi mbalimbali zikiwemo wodi za watoto, akina mama, pamoja na maeneo ya maabara, chumba cha upasuaji na huduma za dharura (EMD), ambapo alijionea namna huduma zinavyotolewa kwa weledi na kwa wakati.
“Nimeridhishwa sana na hali ya utoaji huduma katika hospitali yetu ya rufaa. Watumishi wanafanya kazi kwa moyo, mazingira ni safi, na huduma zinatolewa kwa wakati. Hii ni ishara njema kuwa sekta ya afya mkoani Shinyanga inaendelea kuimarika,” amesema RC Mhita.
Aidha, RC Mhita aliwahimiza watumishi wa hospitali hiyo kuendelea kutoa huduma kwa weledi, uadilifu na huruma kwa wagonjwa, huku akisisitiza umuhimu wa usafi, nidhamu ya kazi, na matumizi sahihi ya vifaa na rasilimali zilizopo hususan Vifaa kama CT SCAN ambazo hazikuwepo awali.
Mkuu wa Mkoa pia alipongeza jitihada za Serikali kupitia Wizara ya Afya kwa kuendelea kupeleka vifaa tiba na kuimarisha miundombinu ya hospitali hiyo, hali inayosaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza rufaa za wagonjwa kwenda hospitali za mbali.
Kwa upande wake Mganga mfawidhi wa Hospitali hiyo Dkt Luzila John alieleza kuwa mafanikio yaliyopo yanatokana na ushirikiano mzuri baina ya uongozi wa hospitali, watumishi na Serikali ya Mkoa, huku wakiahidi kuendelea kuboresha huduma zaidi kwa wananchi.
Ziara ya RC Mhita katika hospitali hiyo ni sehemu ya utaratibu wake wa kutembelea taasisi mbalimbali za umma ili kujionea hali halisi ya utoaji wa huduma kwa wananchi na kuhimiza uwajibikaji.
OFISI YA MKUU WA MKOA, MKOA WA SHINYANGA, 04 MTAA WA BOMA
Anuani: P.O.Box 37180,SHINYANGA, TANZANIA
Simu: +255 28 2762222
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@shinyanga.go.tz
Hakimiliki@2018. Mkoa wa Shinyanga. Haki zote zimehifadhiwa