Na Johnson James, Shinyanga
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Mboni Mhita @mboni_mhita , ametoa wito kwa wananchi wote wa mkoa huo kujitokeza kwa wingi kushiriki kwenye Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba 29, 2025, kwa ajili ya kuwachagua viongozi wao wa Serikali wakiwemo Rais, Wabunge na Madiwani.
Akizungumza na Waandishi wa Habari Ofisini kwake leo Oktoba 25, 2025, wakati wa kutoa kauli ya Serikali kuhusu hali ya usalama ya Mkoa, Mhe. Mhita amesema kuwa mchakato wa uchaguzi unaendelea vizuri na kwamba hakuna tishio lolote la kiusalama. Ameongeza kuwa vyombo vyote vya ulinzi na usalama vimejipanga kuhakikisha uchaguzi unafanyika katika mazingira ya utulivu na amani.
“Ninawasihi wananchi wote wenye sifa, mjitokeze kwa wingi kupiga kura. Hii ni haki yenu ya kikatiba na njia muhimu ya kushiriki katika kuamua mustakabali wa taifa letu. Hali ya usalama ni shwari, na tunahakikisha mazingira yote ya kupigia kura yanakuwa salama,” amesema Mhe. Mhita.
Aidha, Mhe. Mhita ameipongeza Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) kwa kuweka vituo vya kupigia kura karibu na makazi ya wananchi, jambo ambalo limeondoa changamoto ya kutembea umbali mrefu, hasa kwa wazee na watu wenye ulemavu.
Uchaguzi huo utahusisha majimbo 7 na kata 130 za Mkoa wa Shinyanga, ambapo maelfu ya wananchi wanatarajiwa kujitokeza kutumia haki yao ya kikatiba kuchagua viongozi watakaowaongoza kwa kipindi cha miaka mitano ijayo.
Amesisitiza kuwa Serikali itaendelea kuwa bega kwa bega na wananchi kuhakikisha wanashiriki uchaguzi kwa amani, utulivu na mshikamano, huku akisisitiza kuwa yeyote atakayejaribu kuvuruga mchakato huo atachukuliwa hatua kali za kisheria.
OFISI YA MKUU WA MKOA, MKOA WA SHINYANGA, 04 MTAA WA BOMA
Anuani: P.O.Box 320, 37180,SHINYANGA, TANZANIA
Simu: +255 28 2762222
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@shinyanga.go.tz
Hakimiliki@2018. Mkoa wa Shinyanga. Haki zote zimehifadhiwa