Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Mboni Mhita @mboni_mhita leo Oktoba 13, 2025, amewapokea rasmi Madaktari Bingwa 36 kutoka Wizara ya Afya waliowasili mkoani humo kwa ajili ya kutoa huduma za kibingwa katika hospitali zote sita za halmashauri za mkoa huo. Huduma hizo zitafanyika kwa muda wa siku tano, kuanzia Oktoba 13 hadi 17, 2025.

Akizungumza katika hafla fupi ya mapokezi iliyofanyika katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mhe. Mhita aliwashukuru na kuwakirimu madaktari hao huku akibainisha kuwa ujio wao ni sehemu ya dhamira ya Serikali ya awamu ya Sita kusogeza huduma za afya karibu na wananchi na kupunguza msongamano wa wagonjwa kwenye hospitali za rufaa.
Aliongeza kuwa Serikali ya Mkoa itaendelea kuhamasisha wananchi kujitokeza kwa wingi ili kufanyiwa uchunguzi, kupewa tiba na ushauri wa kitaalamu kuhusu magonjwa mbalimbali, hususan yale yanayohitaji huduma za kibingwa.

Awali Katibu Tawala wa Mkoa wa Shinyanga CP Salum Hamdun amesema madaktari hao 36 watahudumu kwenye hospitali za halmashauri sita za mkoa huo na kwamba uwepo wa madaktari hao ni juhudi za serikali za kusogeza huduma kwa wananchi.
Kwa upande wake, Mratibu wa Madaktari Bingwa kutoka Ofisi ya Rais – TAMISEMI Michel Mbele aliwahakikishia viongozi wa Mkoa kuwa timu hiyo imejipanga kutoa huduma bora na za kitaalamu kwa kipindi chote cha siku tano. Amesema lengo ni kuhakikisha wananchi wanapata huduma stahiki na kwa wakati huku pia wakijenga uwezo wa watumishi wa afya waliopo katika vituo husika.
Huduma zitakazotolewa ni pamoja na magonjwa ya wanawake na uzazi, watoto wachanga, magonjwa ya ndani, huduma za upasuaji, usingizi na ganzi, pamoja na huduma za kinywa na meno.
Mpaka sasa, kupitia mizunguko mitatu iliyopita ya programu hii ya kitaifa, zaidi ya wananchi 230,524 wamenufaika na huduma za kibingwa, huku watumishi wa afya 15,019 wakijengewa uwezo katika maeneo mbalimbali nchini, ikiwa ni pamoja na Mkoa wa Shinyanga.
OFISI YA MKUU WA MKOA, MKOA WA SHINYANGA, 04 MTAA WA BOMA
Anuani: P.O.Box 320, 37180,SHINYANGA, TANZANIA
Simu: +255 28 2762222
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@shinyanga.go.tz
Hakimiliki@2018. Mkoa wa Shinyanga. Haki zote zimehifadhiwa