Na Johnson James, Shinyanga
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Mboni Mhita, amezindua rasmi Mpango wa Kitaifa wa Ugawaji wa Mbegu Bora kwa Wakulima kwa mpango wa ruzuku kwa msimu wa kilimo 2025/2026, unaolenga kuongeza tija ya uzalishaji, kukuza uchumi wa wakulima na kuongeza pato la Serikali.
Uzinduzi huo umefanyika leo, Oktoba 23, 2025, katika Ukumbi wa Mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali, taasisi za umma na binafsi, wafanyabiashara, pamoja na wakulima wa mazao mchanganyiko kutoka maeneo mbalimbali ya mkoa huo.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mhe. Mhita alisema kuwa kwa msimu wa kilimo wa mwaka 2025/2026, jumla ya tani 192 za mbegu bora za mazao ya choroko, mbaazi, ufuta, dengu na soya zenye thamani ya shilingi bilioni 1.82 zitanunuliwa na kusambazwa nchini kote.
Kwa Mkoa wa Shinyanga pekee, jumla ya tani 3 za mbegu za choroko zitatolewa na kusambazwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga, Manispaa ya Shinyanga na Halmashauri ya Kishapu ili kuwawezesha wakulima kuongeza uzalishaji na kuboresha kipato chao.
“Ni furaha kubwa kuona mpango huu unatekelezwa kwa vitendo. Tani 192 za mbegu bora zitagawiwa nchini kote, na mkoa wetu utapata tani 3 zitakazowanufaisha wakulima wetu. Hii ni fursa ya kuongeza uzalishaji na kuinua uchumi wa wananchi wetu,” alisema Mhe. Mhita.
Ameeleza kuwa mpango huo ni sehemu ya utekelezaji wa dira ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika kuhakikisha kilimo kinakuwa uti wa mgongo wa uchumi wa taifa kupitia upatikanaji wa mbegu bora, pembejeo za kilimo na masoko ya uhakika kwa wakulima.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Nafaka na Mazao Mchanganyiko (COPRA), Bi. Ireen Mlolwa alisema mamlaka hiyo inaendelea kuhakikisha wakulima wanapata mbegu zenye ubora na tija, zitakazowawezesha kuzalisha mazao bora yenye soko la uhakika ndani na nje ya nchi.
Bi. Mlolwa aliongeza kuwa COPRA kwa kushirikiana na maafisa ugani na vijana waliopitia programu ya Building a Better Tomorrow (BBT) wataendesha mafunzo ya kuwajengea uwezo wakulima kuhusu mbinu bora za kilimo, matumizi ya mbegu bora na upatikanaji wa masoko yenye faida.
Aidha, aliwahimiza wakulima kujiunga na mifumo rasmi ya stakabadhi ghalani ili kupata fursa ya kuuza mazao yao kwa bei bora na kuepuka hasara zinazotokana na biashara zisizo rasmi.
Kwa ujumla, Mkoa wa Shinyanga umeahidi kuendelea kuboresha sekta ya kilimo kama sehemu ya utekelezaji wa maelekezo ya Serikali ya kufanya kilimo kiwe nguzo kuu ya uchumi wa Taifa.
OFISI YA MKUU WA MKOA, MKOA WA SHINYANGA, 04 MTAA WA BOMA
Anuani: P.O.Box 320, 37180,SHINYANGA, TANZANIA
Simu: +255 28 2762222
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@shinyanga.go.tz
Hakimiliki@2018. Mkoa wa Shinyanga. Haki zote zimehifadhiwa