Na. Shinyanga RS.
MKUU wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Christina S. Mndeme amekagua utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga na kubaini uwepo wa uzembe na mianya ya rushwa, na kuwaagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Shinyanga kuchunguza mradi wa ujenzi wa Kituo cha Afya Salawe na kuchukua hatua stahiki kwa yeyote atakayekuwa amehusika.
Mhe. Mndeme ametoa agizo hili alipokuwa akifanya majumuisho ya ukaguzi wa miradi inayosimamiwa na Halmashauri, ambapo kwa upande wa Kituo cha Afya Salawe kilipewa zaidi Tzs. Bil. 1 lakini kimeshindwa kumaliza jengo huku kukiwa na malalamiko kutoka kwa wananchi, uongozi wa Kijiji na Kata juu ya uwepo wa hali ya sintofahamu ya utekelezaji wa mradi huku taarifa kuwa mradi umebakiwa na akiba ya Tzs. 1,300/=
"Nawaagiza TAKUKURU muanze kuchunguza mradi huu kuanzia leo hapahapa na atakayebainika achukuliwe hatua stahiki, katika hili nawataka TAKUKURU mchunguze mpaka senti 38 zilizosomwa humu kwenye taarifa yao," alisema Mhe. Mndeme.
"Haiwezekani Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan atoe fedha nyingi kiasi hiki halafu watu wachache tu wazembe, wacheze na fedha hizi na kukwamisha maendeleo kwa wananchi wa kata hii ya Salawe halafu serikali ikae kimya, hiki kitu hakiwezi kuvulimika hata kidogo," alisisitiza Mhe. Mndeme.
Kwa upande wake Diwani Kata ya Salawe Mhe. Joseph Buyugu alimueleza Mhe. Mkuu wa Mkoa kuwa, kumekuwa na ukiukwahi mkubwa sana wa taratibu katika utekelezaji wa mradi huu, kwakuwa ilifika wakati zikavunjwa kamati zote za usimamizi na ufuatiliaji wa mradi na kisha kuundwa nyingine bila ushirikishwaji wowote, hivyo yeye na wengine wakaamua kukaa kando.
Awali Mhe. Mndeme alikagua ujenzi wa jengo la utawala ofisi ya mkurugenzi wa Halmashauri ambapo pia kulibainika uzembe mkubwa sana kwa uongozi wa Menejimenti na mkandarasi amabye ni SUMA JKT kwakuwa ilipelekea fedha kurudishwa serikalini kwa kushindwa kuzitumia kwa wakati. Hivyo akaigiza Halmashauri kufikia Mei, 2024 jengo likamilike na kuanza kutoa huduma kwa wananchi haraka.
Boma Street, Mwanza Road
Anuani: P.O.Box 320, Shinyanga
Simu: +255 28 2762222
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@shinyanga.go.tz
Hakimiliki@2018. Mkoa wa Shinyanga. Haki zote zimehifadhiwa