Na. Shinyanga RS.
MKUU wa Mkoa wa Shinyanga Christina Mndeme ameanza ziara yenye lengo la kupokea, kusikiliza na kutatua kero za wananchi huku akiwataka watumishi wa Umma kutekeleza wajibu wao kwa weledi katika kuihudumia jamii yetu.
RC MNDEME ameyasema hayo leo Februari 28, 2024 katika mkutano wa hadhara uliofanyika Soko kuu la Manispaa ya Shinyanga ambapo ameweza kupokea, kusikiliza na kuzipatia majawabu kero mbalimbali ikiwemo migogoro ya Ardhi, mirathi, kazi, mikopo umizi, mafao, utelekezaji watoto, ujenzi wa masoko kutokamilika, kubambikiziwa kesi, umeme, kupanda bei ya sukari, na ubovu wa miundombinu ya barabara hasa ya kutoka Kata ya Ndala kuelekea Hospitali ya Rufaa Mwawaza.
"Nawataka watumishi wote ndani ya Mkoa wa Shinyanga kufanya kazi ya kuwahudumia wananchi kwa weledi zaidi, ikiwemo pia kutatua kero za mnaowahudumia katika maeneo yenu ya kazi", amesema RC MNDEME.
Kando na maelekezo hayo, RC MNDEME pia amewataka watumishi wa Idara ya Ardhi kufanya kazi zao kwa weledi na umakini ili kuepusha migogoro ya ardhi, ikiwamo kutogeuza matumizi ya ardhi kinyume na utaratibu.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Mhe. Johari Samizi akijibu kero ya Mikopo umizi, amewataka wananchi wajiepushe na Taasisi ambazo zinakopesha fedha zisizo na vibali wala kutambulika na BOT, na kwamba watakapopata taarifa za Taasisi isiyo sajiliwa wampatie taarifa.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Christina Mndeme, kesho anatendelea na ziara yake ya kusikiliza kero za wananchi na kuzitafutia ufumbuzi katika Manispaa ya Kahama katika viwanja vya Parking ya Malori Kata ya Majengo.
Boma Street, Mwanza Road
Anuani: P.O.Box 320, Shinyanga
Simu: +255 28 2762222
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@shinyanga.go.tz
Hakimiliki@2018. Mkoa wa Shinyanga. Haki zote zimehifadhiwa