Na. Shinyanga RC.
MKUU wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Christina Solomon Mndeme leo tarehe 19 Septemba ametembelea, kukagua na kuweka Jiwe la Msingi ujenzi wa Kituo cha Afya BULIGE kilichopo Halmashauri ya Msalala Wilaya ya Kahama ambapo pamoja na maelekezo mengine lakini pia amemuagiza Mkuu wa Wilaya ya Kahama Mhe. Mboni Mhita @mboni_mhita kuhakikisha anasimamia utekelezaji wa maelekezo yake ili kufikia tarehe 30 Oktoba, 2023 ujenzi huo uwe umekamilika na kuanza kutolewa kwa huduma za afya wananchi ambao ni zaidi ya elfu 39.
Akizungumza wakati wa tukio hilo lililojumuisha viongozi mbalimbali wa Chama Cha Mapinduzi, Serikali na wananchi Mhe. Mndeme alisema, haiwezekani jambo hili lichukue muda mrefu wakati wananchi wanahitaji kupata huduma na siyo kutazama majengo yaliyojengwa ili tuweze kuwaondolea adha ya kupata huduma hasa akina mama, watoto na wazee ambao ni kundi maalum.
"Nakuagiza Mkuu wa Wilaya Mhe. Mboni kuhakikisha unasimamia maelekezo haya ili ifikapo tarehe 30 Oktoba, 2023 huduma zianze kutolewa hapa ikiwemo Wodi ya kujifungulia akina mama," alisema Mhe. Mndeme.
Kando na maelekezo hayo, pia Mhe. Mndeme ameutaka uongozi wa Kituo hiki kupanda miti kuzunguka eneo lote la Kituo cha Afya kwa ajili ya vivuli, kutunza mazingira na kupendezesha eneo.
Awali akisoma taarifa ya ujenzi wa Zahanati ya Bulige Mganga Mfawidhi Catherine Peter alisema kuwa takribani akina mama 15 hadi 20 hujifungua kila siku katika Zahanati ya Bulige huku akisema kukamilika kwa Kituo hiki kunakwenda kuwa mkombozi wa utoaji huduma katika Kata mbili zenye zaidi ya wakazi elfu 39.
Kata ya Bulige ni moja kati Kata 18 zinazojenga Halmashauri ya Msalala na kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022 Kata ya Bulige peke yake ina wakazi 18.184, na ujenzi huu umeanza Februari 2023 na unatarajiwa kukamilika Oktoba 30, 2023 ambapo unakadiriwa kugharimu zaidi ya Milioni 650.
PICHA NA MATUKIO ZIKIMUONESHA MHE. MNDEME AKIKAGUA PAMOJA MKUTANO WA HADHARA AMEONGOZANA NA VIONGOZI MBALIMBALI
Boma Street, Mwanza Road
Anuani: P.O.Box 320, Shinyanga
Simu: +255 28 2762222
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@shinyanga.go.tz
Hakimiliki@2018. Mkoa wa Shinyanga. Haki zote zimehifadhiwa