MKUU wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Christina Mndeme ameziomba Taasisi zote Mkoani Shinyanga zinazohusika na masuala ya utoaji wa haki kufanya kazi kwa kuzingatia kanuni na sheria za nchi huku akizikumbusha kufuata maadili ya taaluma zao.
RC MNDEME ameyasema hayo leo tarehe 27 Januari, 2024 alipokuwa akizindua Maadhimisho ya Wiki ya Sheria Nchini ambapo kwa Kanda ya Shinyanga yamefanyika katika viwanja vya Zimamoto vilivyopo Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga.
"Naziomba Taasisi zote zinazohusika na masuala ya utoaji wa haki hapa Mkoani Shinyanga mfanye kazi kwa kufuata kanuni na taratibu za nchi na pia kwa mzingatie maadili ya taaluma zenu kwa kufanya hivi mtatoa haki sawa na kwa wakati," amesema Mhe. Mndeme.
Kwa upande wake Mhe. Frank Habibu Mahimbali, Jaji Mfawidhi Mahakama ya Tanzania Kanda ya Shinyanga amesema kuwa, uwepo wa maadhimisho haya unatoa fursa zaidi kwa wananchi kuhudumiwa kwa ukaribu, kwa wepesi, kwa urahisi na kupata elimu na ufumbuzi wa changamoto mbalimbali zinayowakabili na kutoka kwa watumishi wa Mahakama ambao wamejipanga vema zaidi katika viwanja vya Zimamoto Manispaa ya Shinyanga.
Awali RC MNDEME aliongoza maandamano kutoka Mahakama Kuu kuelekea viwanja vya Zimamoto ambapo pia aliongoza mazoezi ya viungo kwa watumishi na wadau wa Mahakama na mwisho alihitimisha kwa kutoa wito kwa wananchi kujitokeza hapo ili wapate elimu, kutatua kero zao na kushiriki vema maadhimisho haya muhimu kwa ustawi wa Taifa letu.
Maadhimisho haya ya Wiki ya Sheria yamezinduliwa rasmi leo tarehe 27 Januari, 2024 yatahitimishwa tarehe 1 Februari, 2024 yakiwa na Kauli Mbiu isemayo "Umuhimu wa dhana ya haki kwa ustawi wa Taifa: Nafasi ya Mahakama kwa wadau katika kuboresha Mifumo Jumuishi wa Haki jinai"
HABARI PICHA
Boma Street, Mwanza Road
Anuani: P.O.Box 320, Shinyanga
Simu: +255 28 2762222
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@shinyanga.go.tz
Hakimiliki@2018. Mkoa wa Shinyanga. Haki zote zimehifadhiwa