MKUU wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Christina Mndeme leo tarehw 18 Desemba, 2023 amefungua mafunzo ya wanachama wa klabu za waandishi wa habari wa mikoa ya Shinyanga, Tabora, Geita na Simiyu kuhusu usambazaji na matumizi ya matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022 huku akiwataka wanahabari kutumia elimu na taaluma zao kuelimisha umma juu ya matumizi sahihi ya matokeo ya sensa katika kujiletea maendeleo.
Wito huu umetolewa katika ukumbi wa mikutano uliopo Karena Hotel Manispaa ya Shinyanga ambapo RC Mndeme ameambatana na Kamishna wa Sensa ya Watu na Makazi Mhe. Anna Makinda ambapo pamoja na maelekezo mengine kwa wanahabri lakini ameipongeza sana Ofisi ya Takwimu ya Taifa (NBS) kwa kuweza kushirikisha makundi yote katika mchakato huu wa sensa likiwemo kundi la waandishi wa habari ambao amewataja kuwa ni wadau muhimu sana waliofanya kazi kubwa ya kutoa elimu na hamasa kabla, wakati na baada ya zoezi la sensa kwa wananchi.
"Nawapongeza sana Ofisi ya Takwimu ya Taifa na Wanahabari wote kwa kufanya kazi kubwa sana kabla, wakati na hata baada ya zoezi la Sensa ya Watu na Makazi kwa wananchi wetu, jambo ambalo limepelekea kuwa na matokeo chanya kwa serikali hongereni sana", alisema RC Mndeme.
Kwa upande wake Kamishna wa Sensa ya Watu na Makazi Mhe. Anna Makinda aliwaeleza wanahabari kuwa, moja kati ya malengo ya mafunzo haya ni kuwajengea uwezo wanahabari juu ya uelewa wa namna ya kuripoti na umuhimu wa matumizi sahihi ya sensa ikiwa ni pamoja na kuongeza na kuimarisha uwazi katika kuelimisha wananchi.
Awali akitoa taarifa kabla ya kumkaribisha Mtakwimu wa Mkoa wa Shinyanga Ndg. Eliud Kamendu ambaye alimuwakilisha Mtakwimu Mkuu alisema, uwepo wa mafunzo haya ni muhimu sana katika kuwajengea uwezo wanahabari kwenye utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku hasa wanaporipoti taarifa zenye takwimu kama vile za watu na makazi.
Huku DC wa Shinyanga Mhe. Johari Samizi akiwasisitiza wanahabari kuzingatia mafunzo yanatolewa ili yakawe yenye tija katika kazi zao.
Boma Street, Mwanza Road
Anuani: P.O.Box 320, Shinyanga
Simu: +255 28 2762222
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@shinyanga.go.tz
Hakimiliki@2018. Mkoa wa Shinyanga. Haki zote zimehifadhiwa