Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Zainab Telack, leo tarehe 05/09/2019 amekutana na Wamiliki pamoja na wakuu wa shule binafsi ofisini kwake, kwa lengo la kudumisha mahusiano na kujadili masuala mbalimbali yanayohusu ustawi wa sekta ya elimu Mkoani hapa.
Mhe. Telack akifungua kikao hicho, amesema alikuwa na kiu ya muda mrefu ya kukutana na wamiliki wa shule ili kukaa pamoja na kuona namna bora ya kuongeza ufaulu wa wanafunzi bila kuathiri taaluma na kutoa watoto wanaokubalika kimataifa.
Amesema kasumba ya kuona shule binafsi ni binafsi ni potofu kwani wanaosoma ni watoto wa Watanzania wote.
Amehimiza kuwa, mila potofu zilizopo katika Mkoa wa Shinyanga zitaondoshwa kwa kuhakikisha elimu bora inatolewa katika shule zote zikiwemo shule binafsi.
Aidha, amewataka wakuu wa shule kuwa wakaguzi wa kwanza wa shule zao pale ambapo Wadhibiti ubora hawajafika kutokana na uhaba.
Amewakumbusha pia, wanafunzi wasirudishwe nyumbani kwa kukosa ada hivyo, kila shule iwe na mkataba madhubuti na wazazi ili waweze kulipa ada kwa sababu kumrudisha mtoto ni kuathiri mtiririko wake kitaaluma.
"Wakuu wa shule tumieni taaluma zenu, hakuna mtoto aliyezaliwa akiwa na akili timamu asiyefundishika, badala ya kumfukuza shule wasilianeni na wazazi" amesema Mhe. Telack.
Wakati huo huo, Mhe. Telack amewakumbusha wote kuhakikisha wanashiriki zoezi la uchaguzi wa viongozi wa Serikali za Mitaa kwa kujiandikisha na kupiga kura na kuwamasisha wananchi wengine kushiriki kwani ni kazi ya wote.
Wamiliki pamoja na wakuu wa shule wakitoa maoni na changamoto katika uendeshaji wa shule zao wamehimiza ushirikiano kati yao na Serikali katika masuala mbalimbali ya kitaaluma.
Vilevile, wamemshukuru Mkuu wa Mkoa kwa kuitisha kikao hicho na kusema kuwa, kimewapa motisha ya kuendelea kufanya vizuri zaidi ambapo wameomba kiwe ni kikao endelevu kitakachofanyika kila mwanzo wa mwaka kwa lengo la kujipanga kufanya vizuri kitaaluma.
Boma Street, Mwanza Road
Anuani: P.O.Box 320, Shinyanga
Simu: +255 28 2762222
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@shinyanga.go.tz
Hakimiliki@2018. Mkoa wa Shinyanga. Haki zote zimehifadhiwa