Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Zainab Telack amemuagiza Mkuu wa Wilaya ya Kishapu Mhe. Nyabaganga Taraba kuwakamata wananchi watakaokaidi maelekezo ya wataalamu wa kilimo ya kulima kitalaamu.
Mhe. Telack ametoa agizo hilo akiwa Wilayani Kishapu katika ziara yake ya kukagua shughuli za kilimo na Elimu atakayoifanya kwenye Halmashauri zote Mkoani hapa.
Telack amesema kuwa, Serikali inaposema wakulima wafuate kanuni za kilimo haina maana ya kutaka kuwatesa bali ni kuona kuwa kwa ardhi kidogo wanafaidika na mazao waliyolima.
‘’ Sasa nimesikia kwamba kuna watu wameambiwa limeni kitaalamu hawataki, wanasubiri kukamatwa, ni sawa na mtu anakwambia vaa nguo au kula chakula hutaki” amesema Mhe. Telack.
Amesema Serikali imekuwa na nia thabiti kabisa ya kuwanyanyua wakulima kutoka walipo waende mbele ndiyo sababu ya kuwafukuza maofisini maafisa kilimo na watendaji wa kata kwenda mashambani kusimamia na kuelekeza wakulima na kazi hiyo wameifanya.
Kwa hali hiyo Mhe. Telack amesema wananchi hao wanakaidi amri halali hivyo wakamatwe.
Awali akitoa taarifa ya utekelezaji wa shughuli za kilimo katika msimu huu, Mkuu wa Wilaya ya Kishapu Mhe. Nyabaganga Taraba amesema kuwa, Wilaya imelenga kulima hekta 173,257 kwa mazao ya chakula na biashara ambapo lengo ni kuvuna tani 333,380.
Mhe. Taraba amesema kuwa wananchi wamehamasishwa kulima ekari 3 za mazao ya chakula na ekari 3 za mazao ya biashara. Aidha, taasisi kama shule pamoja na watumishi wamehamasishwa kulima pia.
Amesema pia kuwa Wilaya imejiwekea mikakati mbalimbali kuhakikisha Wilaya haipati tatizo la njaa ikiwemo kuwaelimisha wakulima kuhifadhi chakula na kuacha kutumia kwa mahitaji yasiyo ya lazima kama kutengenezea pombe.
Boma Street, Mwanza Road
Anuani: P.O.Box 320, Shinyanga
Simu: +255 28 2762222
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@shinyanga.go.tz
Hakimiliki@2018. Mkoa wa Shinyanga. Haki zote zimehifadhiwa