Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Zainab Telack amewapa siku 2 wakaguzi kutoka shirika la ukaguzi na usimamizi wa vyama vya ushirika COASCO kutoa sababu za kufanya ukaguzi kinyume cha maelekezo ya Ofisi yake katika Chama Kikuu cha Ushirika SHIRECU.
Mhe. Telack amewaagiza wakaguzi hao leo tarehe 27/10/2018 wakati akifungua Mkutano Mkuu wa mwaka wa Chama cha Kurugenzi SACCOS kinachojumuisha Watumishi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa na Manispaa ya Shinyanga.
Akitoa agizo hilo,Mhe. Telack amegeuka mbogo na kusema kuwa COASCO walielekezwa maeneo ya kufanyia ukaguzi katika chama cha SHIRECU na kuwasilisha matokeo ndani ya siku 8, lakini imebainika kuwa SHIRECU imewapatia wakaguzi hao sh. Milioni 20 bila maelezo yoyote na badala yake ukaguzi huo ufanyike kwa siku 25, kitu ambacho ni kinyume na maelekezo ya Ofisi yake.
"Sitaki blabla ndani ya Mkoa wangu, nataka mnipe majibu kwa nini mnafanya ukaguzi kinyume na maelekezo"
Aidha, Mhe. Telack amewataka watumishi ambao ni wanachama wa Kurugenzi SACCOS kutumia chama hicho kwa manufaa yao na kuwekeza ili kujiongezea kipato.
Wakijadili mambo mbalimbali katika mkutano huo,wanachama wameutaka uongozi kuwa makini katika kuendesha chama hususani katika uandaaji na utunzaji wa taarifa, baada ya kugomea taarifa ya ukaguzi wa hesabu za chama kwa madai kuwa taarifa ya Bodi ya chama ina kasoro hivyo haikuwepo Mkutanoni.
Boma Street, Mwanza Road
Anuani: P.O.Box 320, Shinyanga
Simu: +255 28 2762222
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@shinyanga.go.tz
Hakimiliki@2018. Mkoa wa Shinyanga. Haki zote zimehifadhiwa