Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Zainab Telack amewasilisha changamoto ya kukosekana umeme wa uhakika katika baadhi ya maeneo Mkoani hapa kwa Naibu Waziri wa Nishati Mhe. Subira Mgalu (MB) mapema leo, Ofisini kwake.
Mhe. Telack amesema kuwa kwa upande wa Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga na Mji wa Kahama suala la umeme bado ni changamoto kwani sehemu za pembezoni hakuna umeme wakati ni umbali mdogo kutoka katikati ya mji.
Amemuomba Mhe. Naibu Waziri kuliangalia suala hilo na kumuhakikishia kuwa, iwapo kutakuwa na umeme pembezoni mwa miji hii, Shirika la umeme TANESCO litaongeza mapato yake ya kila mwezi kutokana na kuongezeka kwa matumizi ya umeme, aidha itasaidia kukuza uwekezaji wa shughuli mbalimbali na kuongeza uchumi.
Aidha, Mhe. Telack ameutaka uongozi wa TANESCO Mkoa wa Shinyanga kuwasikiliza wananchi na kushirikiana na Ofisi yake wakati wowote kwa masuala mbalimbali kwa lengo la kuwasaidia wananchi wa Mkoa wa Shinyanga.
Mhe. Naibu Waziri Subira Mgalu amepita Ofisini kwa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga kwa lengo la kumsalimia baada ya ziara yake ya kukagua utekelezaji wa miradi ya REA Mkoani hapa.
Boma Street, Mwanza Road
Anuani: P.O.Box 320, Shinyanga
Simu: +255 28 2762222
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@shinyanga.go.tz
Hakimiliki@2018. Mkoa wa Shinyanga. Haki zote zimehifadhiwa