Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Zainab Telack amewataka Wakuu wa Wilaya hususani za Kahama na Shinyanga kuhakikisha wanasimamia ukusanyaji wa mapato na kutafuta vyanzo vipya vya mapato katika Wilaya zao.
Mhe. Telack ametoa agizo hilo mapema leo wakati wa hafla fupi ya kumuapisha Mkuu mpya wa Wilaya ya Shinyanga Mhe. Jasinta Venant Mboneko katika Ukumbi wa Mikutano wa Ofisi yake.
Amesema kuwa, kazi kubwa waliyonayo Wakuu wa Wilaya ni kusimamia ukusanyaji wa mapato na kutafuta vyanzo vipya "Tupo zamu kumsaidia Mhe. Rais kuyasimamia yote aliyoyapanga lengo ni kuhakikisha tunatekeleza yote yaliyoainishwa katika Ilani" amesema Mhe. Telack.
Telack amewataka pia Wakuu hao wa Wilaya ambao wameteuliwa hivi karibuni kuhakikisha ujenzi wa miradi mbalimbali unakamilika kwa viwango vinavyotakiwa vikiwemo vituo vya Afya, lakini pia kuimarisha hali ya ulinzi na usalama wa Wilaya za Kahama na Shinyanga na kukataa kurubuniwa kwa rushwa ya aina yoyote.
Wakati huo huo Mkuu wa Mkoa Mhe. Telack ametoa rai kwa viongozi wa Dini kuendelea kuomba dua na sala ili kudumisha amani katika Mkoa wa Shinyanga.
" Sala na dua ni muhimu sana, watu wanasema Shinyanga imetulia, haitulizwi na Mkuu wa Mkoa au Mkuu wa Wilaya pekee, bali ni kwa sala na dua zenu" amesisitiza Mhe. Telack.
Aidha, Mkuu wa Wilaya ya Kahama Mhe. Anamringi Macha akijitambulisha rasmi kwa viongozi na watendaji amesema kipaumbele chake cha kwanza katika Wilaya ya Kahama ni kuhakikisha Kahama inakuwa sehemu salama ya kila mtu kuishi.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Kishapu Mhe. Nyabaganga Taraba amewakaribisha Wakuu wa Wilaya za Kahama na Shinyanga na kuwahimiza ushirikiano na kumtegemea Mungu katika kutekeleza vema majukumu yao.
Viongozi mbalimbali wakiwemo wa Dini, Vyama vya Siasa na Watendaji pia wakitoa salamu zao katika hafla hiyo, wamewakaribisha Wakuu hao wa Wilaya na kuwaahidi ushirikiano katika kipindi chote watakachokuwa katika Mkoa huu.
Boma Street, Mwanza Road
Anuani: P.O.Box 320, Shinyanga
Simu: +255 28 2762222
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@shinyanga.go.tz
Hakimiliki@2018. Mkoa wa Shinyanga. Haki zote zimehifadhiwa