Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Zainab Telack amepiga marufuku bidhaa za vyakula kuuzwa zikiwa nje ya maduka hali inayochangia bidhaa hizo kupigwa na jua hivyo kupoteza ubora na kugeuka sumu kwa watumiaji.
Mhe. Telack ametoa marufuku hiyo huku akiwataka Maafisa Afya kusimamia suala hilo katika kikao cha maandalizi ya mpango wa Bajeti ya lishe kwa mwaka 2020 /2021 kilichofanyika Jumatatu ya tarehe 02 Desemba, 2019 Ofisini kwake.
Amesema Maafisa Afya wakisimama katika nafasi zao wataweza kuhakikisha wananchi wanakula vyakula vyenye ubora na kupunguza hatari ya maradhi yanayotokana na sumu za vyakula vilivyopigwa jua.
Aidha, Mhe. Telack amehimiza elimu ya lishe kuanzia utungaji wa mimba hadi miaka mitano kwa watoto itolewe katika kila Kituo cha Afya kabla ya kuwapima akina mama wajawazito, ili wananchi wapate uelewa na kupunguza tatizo la udumavu katika Mkoa.
Amesema kama watoto watalishwa vizuri suala la udumavu litapungua na kwisha kabisa hivyo kupunguzia Serikali bajeti kubwa ya dawa inayoongezeka kila mwaka.
"Serikali inaongeza bajeti ya dawa kila siku kwa sababu watu hawali vizuri wanaugua, tusipoangalia suala hili tutakuwa na Taifa la lenye watu wadumavu ndiyo maana Serikali imelishikia bango" amesema Telack.
Naye Mratibu wa Lishe kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI Bw. Mwita Waibe amesema kuwa, nchi inatumia fedha nyingi sana kwenye matibabu na vifaa tiba ikiwemo dawa, vitanda, mashuka na vifaa vya Maabara kwa sababu tu ya ukosefu wa lishe duni.
Afisa Lishe kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI, Bw. Japhari Magesa akiwasilisha mada ya umuhimu wa lishe amesema kuwekeza katika lishe ni muhimu kwa kuongeza kiwango cha uelewa na ufaulu katika Elimu huku akitoa takwimu kuwa watoto wenye udumavu duniani ni milioni 151 huku watoto wenye udumavu Tanzania ni milioni 3.
Boma Street, Mwanza Road
Anuani: P.O.Box 320, Shinyanga
Simu: +255 28 2762222
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@shinyanga.go.tz
Hakimiliki@2018. Mkoa wa Shinyanga. Haki zote zimehifadhiwa