Waajiri wa sekta binafsi Mkoani Shinyanga wameagizwa kuhakikisha wanafuata sheria za kazi ikiwemo kuwapatia mikataba ya kazi ya maandishi watumishi wao pamoja na vitendea kazi ili waweze kufanya kazi katika hali ya usalama.
Agizo hilo limetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Zainab Telack wakati wa maadhimisho ya siku ya Wafanyakazi Duniani ambayo kimkoa imefanyika katika uwanja wa Kambarage, Manispaa ya Shinyanga.
Mhe. Telack amemuagiza Katibu Tawala Mkoa kuunda kamati itakayofuatilia utekelezaji wa agizo hilo na kumpatia taarifa.
“Naagiza waajiri wote wa sekta binafsi wiki mbili kuanzia leo kufuata sheria za kazi na
tarehe 15/05/2017 Katibu Tawala Mkoa ataunda kamati ndogo kupitia sekta zote kama wametekeleza maagizo”.
Kuhusu suala la Sekta binafsi kutojali sheria ya Wafanyakazi, Mkoa umekuwa ukiwaagiza wamiliki na watendaji kuzingaria sheria ya ajira na mahusiano kazini mara kwa mara.
Aidha, Mhe. Telack amesema, Serikali inatekeleza kwa vitendo uwezeshaji katika uanzishaji wa viwanda vikubwa na vidogo hivyo wananchi wote tunapaswa kufanya kazi kwa bidii katika kutoa huduma na bidhaa bora ili kuweza kupata malighafi kwa viwanda vinavyoanzishwa.
“Wafanyakazi bado tunayo fursa ya kujihusisha na kilimo ili kuongeza malighafi,walau kila mfanyakazi awe na ekari moja, hii itapunguza wafanyakazi kuwa wanunuaji tu bali washiriki katika uzalishaji”.
Amesema kuwa, Mkoa umekuwa kivutio cha uwekezaji wa viwanda kutokana na huduma zote muhimu, umeme, maji, amani, utulivu na ukarimu wa wananchi.
Amewataka wafanyakazi na wananchi wote kuwajibika katika kulinda amani na utulivu kwani ni muhimu kwa maendeleo ya Mkoa na nchi kwa ujumla.
Mhe. Mkuu wa Mkoa, ametoa rai kwa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (TUCTA) kuendelea kutoa ushirikiano chanya kwa Serikali na Wafanyakazi. Aidha wafanyakazi watambue kuwa, kuna haki na wajibu hivyo, watumie muda mwingi kutimiza wajibu wao wa kuhudumia wananchi kuliko kulalamika na wachache ambao ni wazito, TUCTA iendelee kuwakumbusha wajibu wao.
Boma Street, Mwanza Road
Anuani: P.O.Box 320, Shinyanga
Simu: +255 28 2762222
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@shinyanga.go.tz
Hakimiliki@2018. Mkoa wa Shinyanga. Haki zote zimehifadhiwa