Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu amewahakikishia wanafunzi wa chuo cha ualimu Shinyanga (SHYCOM) kuwa Serikali itatatua changamoto zao zinazowakabili ili wasome katika mazingira mazuri.
Akizungumza na wanafunzi wa chuo hicho katika ziara yake Mkoani Shinyanga mapema leo tarehe 27 /02/2019, Mhe. Samia amemuagiza Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi kuhakikisha changamoto zilizotajwa na wanafunzi hao ikiwemo maji na maktaba zinashughulikiwa haraka.
Ikiwa ni siku ya pili ya ziara yake, Mhe. Samia amekagua ujenzi wa Ofisi ya Mamlaka ya Maji Kahama na Shinyanga (KASHWASA) inayojengwa na Serikali kuu kwa gharama ya sh. Bil. 1.7 ambayo ujenzi wake umefika asilimia 85 na inatarajiwa kuanza kazi mwezi Mei mwaka huu.
Wakati huo huo, Mhe. Samia amefungua pia bwalo la chakula katika shule ya msingi Buhangija na kuwaomba wadau mbalimbali kuendelea kusaidia kupunguza changamoto kama ilivyofanya kampuni ya Simba Logistics kujenga bwalo hilo.
Naibu Waziri Ofisi ya Rais TAMISEMI Mhe. Mwita Waitara, ameahidi kushughulikia suala la uzio katika shule hiyo kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu kwa namna yoyote ile.
Naye Naibu Waziri wa Elimu aliyeambatana na Mhe. Samia amesema kuwa Wizara ya Elimu inafanyia kazi suala la kuongeza walimu hasa wa wanafunzi wa mahitaji maalumu kwa kuongeza udahili wa walimu wa masomo hayo na kuongeza mikopo ya elimu ya juu kwa walimu hao.
Boma Street, Mwanza Road
Anuani: P.O.Box 320, Shinyanga
Simu: +255 28 2762222
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@shinyanga.go.tz
Hakimiliki@2018. Mkoa wa Shinyanga. Haki zote zimehifadhiwa