Serikali Mkoani wa Shinyanga imekamata mifuko ya bandia zaidi ya elfu 20 yenye nembo za makampuni ya sukari Nchini inayotumika kubeba sukari isiyokuwa na viwango na kuisambaza kwenye masoko wakati sukari ya viwanda inayozalishwa na viwanda vya ndani ya nchi haitoki kwenye viwanda.
Mifuko hiyo imekamatwa kupitia kikosi kazi maalumu kilichoundwa na Mkoa ili kuendelea na zoezi lililoanza Mwezi Oktoba mwaka jana 2018 lenye lengo la kuwakamata wahujumu uchumi Mkoani hapa.
Akitoa taarifa ya zoezi hilo mapema leo tarehe 1 Julai, 2019 mbele ya waandishi wa Habari, Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Zainab Telack amesema kutokana na taarifa za raia wema, watu 14 akiwemo raia mmoja wa kigeni wamekamatwa katika Wilaya za Kahama, Nzega, Igunga na Mkoani Arusha kwa makosa ya uhujumu uchumi ikiwemo kutengeneza, kuuza na kumiliki mifuko na vifungashio bandia.
Mhe. Telack amesema mifuko hiyo ya kampuni tofauti ikiwemo ya Kagera Sugar na Kilombero Sugar, kama ingeingia sokoni ingeweza kupakiwa sukari tani 1000 yenye thamani ya shilingi bilioni 2 na kuwa, viwanda vya ndani visingeweza kuzalisha.
"Sukari hii ingeingia kwenye soko maana yake ni kwamba, hivi viwanda vya ndani visingeweza kuzalisha kwa sababu sukari ambayo haijulikani inatoka wapi ipo sokoni, kitendo hiki ni uhujumu uchumi na kukwamisha juhudi za Serikali za kulinda viwanda vya ndani" amesema Telack.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga ACP Richard Abwao amesema kuwa, raia wa kigeni ndiye amekamatwa katika Mkoa wa Arusha kwa kosa la uingizaji wa mifuko hiyo inayodhaniwa kutengenezwa katika kiwanda kimoja cha nchi ya jirani na tayari watuhumiwa wote wamefikishwa mahakamani Mkoani Shinyanga na Tabora.
Telack amewataka wananchi watoe taarifa endapo wakiona kuna watu wanafanya biashara za kuuza bidhaa zisizojulikana, Mkoa una kikosi kazi ambacho kipo tayari kwenda Mkoa wowote.
Boma Street, Mwanza Road
Anuani: P.O.Box 320, Shinyanga
Simu: +255 28 2762222
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@shinyanga.go.tz
Hakimiliki@2018. Mkoa wa Shinyanga. Haki zote zimehifadhiwa