Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Zainab Telack akiwa na Kamati za Usalama za Mkoa na Wilaya ya Shinyanga amekamata jumla ya kadi za kutolea fedha 267za benki tofauti ambazo ni mali ya Watumishi wa Umma wa Mkoa wa Shinyanga pamoja na kadi za bima za afya, vitambulisho vya kazi na vitambulisho vya kupigia kura katika taasisi ya kukopesha fedha ya Mara Credit Co, Ltd (MCCL) iliyopo katika Manispaa ya Shinyanga, leo tarehe 04 Mei, 2019.
Taasisi hiyo inayojihusisha na kukopesha fedha kwa watumishi wa Umma na watu binafsi kwa kuchukua kadi zao na namba za siri kwa lengo la kutoa fedha kwenye akaunti zao mshahara unapoingia, imebainika pia kuwakamata watumishi wa umma na kuwafungia kwenye chumba ndani ya Ofisi hiyo pale wanaposhindwa kulipa madeni yao.
Meneja wa taasisi ya hiyo Bw. Cleophace Steven amehojiwa na kukiri kuwa, wanatoa mikopo na kuchukua kadi za watumishi kwa lengo la kutoa fedha kwenye akaunti za wadaiwa wao.
Mhe. Telack akifanya ukaguzi wa Ofisi hiyo, amewaagiza waajiri wote wa taasisi za Umma kusimamia watumishi wao na kuhakikisha kadi zao za kutolea fedha wanazo na kama zipo kwenye taasisi za kukopesha fedha zitakamatwa.
“Naahidi watumishi wa Mkoa huu watafanya kazi bila msongo wa mawazo, nyie mnawatengenezea msongo wanashindwa kufanya kazi kwa amani, nawaambia kwenye Mkoa huu nafasi hiyo haipo! masharti yaliyoanzisha taasisi zenu hayakuwaambia mfanye hivyo” amesema Mhe. Telack.
Amemtaka pia Katibu Tawala Mkoa kuhakikisha anapata orodha ya watumishi wote ambao kadi zao zipo kwenye taasisi za kukopesha fedha na watu binafsi wanaokopesha fedha.
Aidha amemtaka meneja wa Mamlaka ya Mapato Mkoa kuwasilisha taarifa Ofisini kwake inayoonesha mapato yanayopatikana kutokana na biashara hiyo.
Boma Street, Mwanza Road
Anuani: P.O.Box 320, Shinyanga
Simu: +255 28 2762222
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@shinyanga.go.tz
Hakimiliki@2018. Mkoa wa Shinyanga. Haki zote zimehifadhiwa