Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Dkt. Faustine Ndugulile amemuagiza Katibu Mkuu wa Wizara hiyo kuhakikisha Mikoa yote inaunda mabaraza ya Wazee na kuwapa nyenzo muhimu kwa ajili ya shughuli zao kabla ya Mwaka huu kuisha.
Mhe. Ndugulile ametoa agizo hilo jana wakati akizindua rasmi jengo la makazi ya Wazee katika kata ya Kolandoto, Manispaa ya Shinyanga.
Mhe. Ndugulile amesema kuwa, Serikali ina mikakati mbalimbali ya kuwaenzi Wazee ili kupata busara na ushauri wao ndiyo maana kumeanzishwa mabaraza ya Wazee.
Ameipongeza Serikali ya Mkoa wa Shinyanga kwa kufanya vizuri kuanzisha mabaraza ya Wazee kuanzia ngazi ya kijiji hadi Mkoa na kuwapatia vitendea kazi ikiwepo Ofisi.
“Nitumie fursa hii kukumbusha Mikoa mingine ambayo bado haijaanzisha mabaraza ya Wazee ifanye hivyo mara moja, ni agizo la Serikali tunataka mabaraza ya Wazee kwenye kila Mkoa ndani ya nchi yetu na kuwapatia nyenzo za kufanya kazi” amesema Mhe. Ndugulile.
Mhe. Ndugulile pia amesisitiza agizo la kuhakikisha wazee wote wenye umri wa miaka 60 na kuendelea wanapatiwa kadi za matibabu, kila kituo cha kutolea huduma za Afya kuweka madirisha ya tiba kwa wazee na kuwapa kipaumbele wanapofika kwenye vituo hivyo.
Aidha, amempongeza Katibu Mkuu kwa usimamizi mzuri wa jengo bora kwa ajili ya wazee wasiojiweza katika kata ya Kolandoto na ukarabati wa miundombinu muhimu.
Awali akitoa shukrani kwa Mhe. Naibu Waziri, mwenyekiti wa Baraza la Wazee Mkoa wa Shinyanga ndg. Faustine Sengerema ameiomba Serikali kuona uwezekano wa kupitia upya Sheria ya kulinda maslahi ya Wazee nchini.
Boma Street, Mwanza Road
Anuani: P.O.Box 320, Shinyanga
Simu: +255 28 2762222
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@shinyanga.go.tz
Hakimiliki@2018. Mkoa wa Shinyanga. Haki zote zimehifadhiwa