Waziri wa Kilimo Mhe. Japhet Hasunga amesema Serikali ya Tanzania kupitia Benki kuu, imeamua kuweka dhamana kwa kufidia hasara itakayopatikana kwa wanunuzi wa Pamba kwenye soko la Dunia ili waweze kununua Pamba kwa bei ya shilingi 1,200 kwa kilo.
Akizungumza na Viongozi wa Mkoa na Wakulima kwa nyakati tofauti leo tarehe 15/07/2019 wakati akianza ziara ya siku tatu Mkoani Shinyanga Mhe. Hasunga amesema Serikali imefikia maamuzi hayo katika kikao cha pamoja kati ya Serikali, wanunuzi na baadhi ya wamiliki wa Benki kilichoitishwa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa Mkoani Tabora jana tarehe 14/07/2019.
"Kuanzia leo, Benki kuu itakuwa inakamilisha taratibu zote na wafanyabiashara wataanza kupewa fedha kwa ajili ya kununua pamba" amesema Mhe. Hasunga.
Aidha, amezidi kueleza kuwa, Serikali imezitaka Benki kupunguza riba kutoka asilimia 16 hadi asilimia 11 ili kuwawezesha wanunuzi kupata fedha za kununua pamba.
Hasunga amesema lengo la Serikali ni kuwasaidia wanunuzi waweze kupata fedha ya kununua pamba yote ya wakulima na wakulima wapate fedha kwa bei ya shilingi 1,200 kwa kilo kama ilivyotangazwa licha ya bei ya soko la Dunia kushuka.
Amewahakikishia wakulima kuwa, vituo vyote kutakuwa na fedha za kutosha kununua pamba na wakulima watapata fedha zao moja kwa moja na pia kuanzia mwaka ujao kutakuwa na mfumo mzuri zaidi wa ununuzi wa pamba usiokuwa na usumbufu kwa wakulima na wanunuzi.
Akielezea changamoto zilizotokana na wanunuzi kushindwa kununua pamba katika msimu huu, Mhe. Hasunga amesema kuwa Serikali ilitangaza bei ya sh. 1,200 kwa kilo baada ya kukokotoa na wanunuzi na kuona bei katika soko la Dunia ipo juu, lakini kutokana na vikwazo mbalimbali bei ya soko la Dunia imeshuka hivyo wakulima watapata hasara iwapo watanunua kwa bei hiyo, pia Benki zilikataa kuwapa fedha kwa kubaini hasara hiyo.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Zainab Telack amebainisha kuwa, Shinyanga ndiyo Mkoa wenye viwanda vinavyomilikiwa na wazawa ni vema pia kuzungumza na wenye viwanda hivi kufahamu wanahitaji kiasi gani ili waweze kununua pamba inayozalishwa Mkoani hapa.
Akizungumza na wakulima katika kiwanda cha Afrisian kilichopo Manispaa ya Shinyanga, Mhe. Telack amewataka wakulima kuhakikisha wanaitunza vizuri pamba ili isishuke ubora wake, kwani pamba ya Tanzania inasifika kwa ubora na nyuzi zinazofaa kwa kutengeneza nguo.
Mhe. Hasunga yupo Mkoani Shinyanga kwa siku tatu ikiwa ni ziara ya kikazi, pamoja na shughuli nyingine atatembelea vituo vya kununulia pamba.
Boma Street, Mwanza Road
Anuani: P.O.Box 320, Shinyanga
Simu: +255 28 2762222
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@shinyanga.go.tz
Hakimiliki@2018. Mkoa wa Shinyanga. Haki zote zimehifadhiwa