Na. Shinyanga RS.
Serikali imeitaka Kampuni ya China Hennan International Corperation Group Co. Ltd (CHICO) iliyopewa kandarasi ya kufanya maboresho makubwa katika Uwanja wa Ndege wa Mkoa wa Shinyanga inatekeleza kazi hiyo na kukabidhi ndani ya muda uliopangwa.
Hayo yamesemwa na mgeni rasmi Mhe. Johari Samizi Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga aliyemuwakilisha Mhe. Christina Mndeme ambaye ni Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga katika Hafla ya Utambulisho wa Mradi wa Maboresho ya uwanja huo yaliyofanyika katika eneo la Ofisi ya Uwanja wa Ndege iliyopo Kata ya Ibadakuli Manispaa ya Shinyanga Mkoa wa Shinyanga na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali akiwamo Katibu Tawala Mkoa wa Shinyanga Pro. Siza D. Tumbo, Kamati za Ulinzi, viongozi wa Dini na wadau mbalimbali wa Usafiri wa Anga.
“Nitoe rai kwa (CHICO) ambaye ndiye mkandarasi wa maboresho haya makubwa ya uwanja wetu wa ndege kuhakikisha anafanya kazi hii kwa weledi, uaminifu, viwango na uzalendo mkubwa huku akizingatia muda uliowekwa na aweze kukabidhi kwa wakati ili wananchi wa Mkoa wa Shinyanga waanze kunufaika na kufurahia huduma hii ambayo kwa sasa wanalazimika kuifuata Mkoa wa Mwanza ambapo hulazimika kutumia Kilomita 164 kutokea hapa Shinyanga,” alisema Mhe. Johari.
Awali akisoma taarifa ya maboresho hayo Meneja Mradi Viwanja vya Ndege – TANROAD Makao Makuu Mhandisi Neema Joseph alisema kuwa mkandarasi atatumia miezi 18 (Aprili, 2023 hadi Oktoba, 2024) na kwamba katika kazi hiyo itakayogharimu zaidi ya Bilioni 49 za Kitanzania fedha zitokanazo na Ufadhili wa Benki ya Uwekezaji kutoka Ulaya.
Kwa upande wake Meneja TANROAD Mkoa wa Shinyanga Mhandisi Mibara Ndirimbi alisema kuwa, pamoja na kazi nyingine lakini mkandarasi atafanya maboresho na kutengeneza barabara ya kuruka na kutua ndege kwa kiwango cha lami, barabara ya kiungio na maegesho ya ngede kwa kiwango cha lami, jengo jipya la kupumzikia abiria lenye uwezo wa kuchukua watu 150 hadi 250 kwa wakati mmoja, barabara ya kuingia uwanjani pamoja na jengo la Huduma za Hali ya Hewa huku akitumia fulsa hiyo kuwataka wananchi wa Mkoa wa Shinyanga kuulinda mradi huo na kuepuka vitendo vyovyote vya hujuma.
“Pamoja na shukurani kwa Serikali yetu, lakini niwaombe pia wananchi wa Mkoa wa Shinyanga kwa umoja wetu tushirikiane katika kuulinda mradi huu bora kabisa kwa maslahi yatu na Taifa ili kusiwepo na vitendo vyovyote vya hujuma na mwisho tuje kunufaika na kufurahia uwepo wa Uwanja huu hapa Shinyanga,” alisema Mhandisi Ndirimbi
Kukamilika kwa mradi huu unaoboreshwa kuwa na urefu wa kilomita 2 na upana wa mita 30 za upana wa njia ya kurukia na kutua kwa ndege kunatajwa kwenda kuwaondelea adha kubwa wanaoyoipata wananchi wa Mkoa wa Shinyanga pamoja na maeneo jirani sambamba na kuongeza mzunguuko wa fedha jambo ambalo litainua uchumi wa mtu mmoja mmoja wa Mkoa na kuongeza pato kwa Taifa kwa ujumla wake.
Picha ikionesha wajumbe wakikagua moja kati ya barabara zitakazotengenezwa na mkandarasi CHICO
Picha ikimuonesha Meneja TANROAD Mkoa wa Shinyanga Mhandisi Mibara Ndirimbi akielezea jambo wakati wa hafla ya utambulisho wa mradi wa uboreshaji wa upanuzi wa uwanja wa ndege
Boma Street, Mwanza Road
Anuani: P.O.Box 320, Shinyanga
Simu: +255 28 2762222
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@shinyanga.go.tz
Hakimiliki@2018. Mkoa wa Shinyanga. Haki zote zimehifadhiwa