Na Johnson James, Shinyanga
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Mboni Mhita @mboni_mhita amewatoa hofu wananchi wa mkoa huo kuhusu hali ya usalama kuelekea Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29, 2025, akisisitiza kuwa mkoa uko salama na hauna tishio lolote la kiusalama.
Akizungumza katika kikao na waandishi wa habari kilichofanyika kwenye ukumbi wa Virgimack Hotel Octoba 20,2025 , Mhe. Mhita amesema Serikali ya Mkoa imejipanga kikamilifu kuhakikisha zoezi la kupiga kura linafanyika kwa amani, utulivu na haki bila bughudha kwa mpiga kura yeyote.
“Natoa rai kwa wananchi wa Shinyanga kujitokeza kwa wingi kutumia haki yao ya kikatiba. Serikali tupo tayari, vyombo vyetu vya ulinzi na usalama vipo macho kuhakikisha siku hiyo inapita kwa amani. Hakuna tishio lolote la kiusalama,” amesema RC Mhita.
Amesisitiza kuwa yeyote atakayebainika kuchochea vurugu au vitendo vinavyoashiria uvunjifu wa amani atachukuliwa hatua kali za kisheria mara moja, ili kulinda utulivu wa mkoa na kuhakikisha kila mwananchi anatekeleza wajibu wake bila hofu.
“Tunaendelea kufuatilia kwa karibu mienendo yote ya kisiasa na kijamii. Hatutamvumilia mtu yeyote atakayevuruga amani. Tunataka uchaguzi uwe wa heshima, utulivu na unaoendana na maadili ya taifa letu,” aliongeza.
Aidha, alisisitiza kuwa amani ni msingi wa maendeleo, na kwamba hakuna mkoa au taifa linaloweza kupiga hatua kiuchumi au kijamii pasipo utulivu.
OFISI YA MKUU WA MKOA, MKOA WA SHINYANGA, 04 MTAA WA BOMA
Anuani: P.O.Box 320, 37180,SHINYANGA, TANZANIA
Simu: +255 28 2762222
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@shinyanga.go.tz
Hakimiliki@2018. Mkoa wa Shinyanga. Haki zote zimehifadhiwa