Zaidi ya vituo 331 vya kutolea huduma za afya katika mkoa wa Shinyanga vinatarajiwa kusajiliwa katika mfumo wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Nchini (TIRA) ikiwa ni sehemu ya maboresho ya huduma kwa wananchi kupitia mpango wa bima ya afya kwa wote.
Zoezi hilo linaendeshwa kwa muda wa Siku tano Mfululizo na na Afisa TEHAMA wa Mkoa wa Shinyanga Bwana Ammy Mohamed, Ofisi ya Mganga Mkuu wa Mkoa kwa kushirikiana na Paul Nicholaus ambaye ni Afisa TEHAMA kutoka Mamlaka ya Usimamizi wa Bima (TIRA) – Kanda ya Magharibi, wakitembelea halmashauri zote sita za mkoa huo.
Kwa mujibu wa Ammy Mohamed, usajili huo utasaidia kuondoa changamoto mbalimbali zilizokuwepo awali kwenye utoaji wa huduma za bima ya afya, sambamba na kuhakikisha upatikanaji wa taarifa sahihi kwa wakati kwa ajili ya kufanya maamuzi ya kitaasisi na kisera.
Kwa upande wake, Paul Nicholaus alibainisha kuwa utekelezaji wa usajili huu ni agizo la Serikali katika kuimarisha mifumo ya Afya ya kidigitali ili kusaidia kufanikisha dira ya taifa ya kufikia bima ya afya kwa wote.
Hatua hii ni sehemu ya dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha kila Mtanzania anapata huduma bora, nafuu na endelevu za afya kupitia mfumo wa bima kwa wote.
OFISI YA MKUU WA MKOA, MKOA WA SHINYANGA, 04 MTAA WA BOMA
Anuani: P.O.Box 37180,SHINYANGA, TANZANIA
Simu: +255 28 2762222
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@shinyanga.go.tz
Hakimiliki@2018. Mkoa wa Shinyanga. Haki zote zimehifadhiwa