Na Johnson James- Shinyanga
Serikali ya Mkoa wa Shinyanga kwa kushirikiana na Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania (TACAIDS), Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Wizara ya Afya, UNICEF na wadau wengine wa maendeleo, imefanya kikao kazi muhimu kwa ajili ya kujadili mikakati ya kuboresha huduma za afya kwa vijana balehe, hasa katika mapambano dhidi ya maambukizi ya Virusi vya Ukimwi (VVU).
Akifungua kikao hicho, Mwakilishi wa Katibu Tawala wa Mkoa wa Shinyanga David Lyamong ambaye ni Katibu Tawala Msaidizi Utawala na Rasilimaliwatu amesema kuwa lengo kuu ni kuhakikisha kundi la vijana balehe linafikiwa na huduma bora za afya zikiwemo za lishe, afya ya akili na afya ya uzazi, ili kulinda afya na mustakabali wa kundi hilo muhimu katika maendeleo ya taifa.
Kwa mujibu wa takwimu za Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022, Mkoa wa Shinyanga una vijana balehe wapatao 449,038 wenye umri wa miaka 15 hadi 24. Hata hivyo, hali ya maambukizi ya VVU kwa kundi hili ni ya juu kwa asilimia 6.2, ukilinganisha na wastani wa kitaifa wa asilimia 3.7. Hali hii imepelekea mkoa kuchukua hatua madhubuti kupitia ushirikiano wa karibu na wadau mbalimbali.
“Tumeendelea kusimamia afua mbalimbali za VVU na UKIMWI katika Halmashauri zote sita za mkoa wetu kwa lengo la kuimarisha afya za vijana balehe. Vijana hawa wanakumbana na changamoto nyingi ikiwa ni pamoja na lishe duni, afya ya akili na afya ya uzazi. Tunajitahidi kuhakikisha wanapata huduma bora, japo ufinyu wa rasilimali bado ni changamoto,” alisema mtoa hotuba.
Katika hatua za awali za utekelezaji, zoezi la usimamizi shirikishi limefanyika kati ya tarehe 15 hadi 16 Oktoba 2025 katika Manispaa za Kahama na Shinyanga pamoja na Halmashauri ya Wilaya ya Msalala. Kazi hii imewezesha kubainisha maeneo yenye mafanikio pamoja na changamoto zinazohitaji suluhisho la haraka.
Kikao kazi hiki kinatarajiwa kuibua maazimio ya pamoja yatakayosaidia kuongeza ufanisi wa utoaji huduma kwa vijana, pamoja na kuweka mikakati endelevu ya kupunguza maambukizi mapya ya VVU miongoni mwa vijana.
Mkoa wa Shinyanga umeahidi kuendelea kushirikiana na TACAIDS na wadau wote wa maendeleo kuhakikisha kuwa juhudi za kukabiliana na VVU/UKIMWI kwa vijana zinaimarika, na hatimaye kufikia kizazi kisicho na maambukizi mapya ya VVU.
OFISI YA MKUU WA MKOA, MKOA WA SHINYANGA, 04 MTAA WA BOMA
Anuani: P.O.Box 320, 37180,SHINYANGA, TANZANIA
Simu: +255 28 2762222
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@shinyanga.go.tz
Hakimiliki@2018. Mkoa wa Shinyanga. Haki zote zimehifadhiwa