Katibu Tawala wa Mkoa wa Shinyanga, CP Salum Hamduni, kupitia mwakilishi wake Bi. Rehema Ambwindwile ambaye ni Afisa Maendeleo ya Jamii Mkoa, ameagiza Wakurugenzi wa Halmashauri na Manispaa zote mkoani humo kuhakikisha wanasimamia kikamilifu udhibiti wa viashiria vya utoro na udondoshaji wa wanafunzi mashuleni.
Bi. Ambwindwile ametoa agizo hilo leo Septemba 4,2025 kwa niaba ya Katibu Tawala wa Mkoa wa Shinyanga wakati wa kilele cha maadhimisho ya Juma la Elimu ya Watu Wazima na Elimu Nje ya Mfumo Rasmi yaliyofanyika katika Uwanja wa Shule ya Msingi Town, Manispaa ya Shinyanga.
Alisema Katibu Tawala amesisitiza kuwa tatizo la wanafunzi kuacha shule lina mchango mkubwa katika kuongeza idadi ya watu wazima wasiojua kusoma, kuandika na kuhesabu (KKK).
Katika kuhakikisha tatizo hilo linakomeshwa, Wakurugenzi wa Halmashauri wametakiwa kuanzisha madarasa ya Kisomo katika kila kata na kuhakikisha yanakuwa endelevu.
Lengo ni kuwajengea uwezo watu wazima waliokosa fursa ya elimu ya awali, ili waweze kushiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi na kijamii.
Awali, akiwasilisha risala kwa niaba ya Afisa Elimu Mkoa wa Shinyanga, Afisa Elimu wa Watu Wazima na Elimu Nje ya Mfumo Rasmi Mkoa, Bw. Dedan Rutazika, alieleza kuwa changamoto kubwa ni ongezeko la wanafunzi wanaoacha shule, hali inayozalisha kizazi kisichokuwa na ujuzi wa msingi wa KKK.
Ambapo pamoja na mambo mengine ameiomba serikali kuingilia kati swala la utoro wa wanafunzi mashuleni amoja na wale wanaoacha shule jambo linalotajwa kwamba litapunguza kizazi cha watu Wazima wasiojua Kusoma na Kuandika katika mkoa wa Shinyanga.
Maadhimisho hayo yalipambwa na maonesho ya bidhaa mbalimbali kutoka kwa wananchi waliopata elimu nje ya mfumo rasmi, wakionesha ufanisi na mchango wa elimu hiyo katika kuimarisha maisha yao ya kila siku.
OFISI YA MKUU WA MKOA, MKOA WA SHINYANGA, 04 MTAA WA BOMA
Anuani: P.O.Box 320, 37180,SHINYANGA, TANZANIA
Simu: +255 28 2762222
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@shinyanga.go.tz
Hakimiliki@2018. Mkoa wa Shinyanga. Haki zote zimehifadhiwa