Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Zainab Telack amepokea magari mawili yenye thamani ya sh. Mil. 189.5 jana tarehe 06/02/2019 kutoka Shirika la AGPAHI, kwa ajili kutoa huduma za masuala ya VVU na UKIMWI katika Halmashauri za Kahama Mji na Ushetu.
Akikabidhi magari hayo kwa Mkuu wa Mkoa, Mkurugenzi Mkazi wa shirika hilo linalojishughulisha na kutokomeza maambukizi ya VVU na UKIMWI hususani kwa watoto, Dkt. Sekela Mwakyusa amesema lengo kubwa ni kusaidia masuala ya ufuatiliaji na kufikisha huduma kwa jamii.
Dkt. Mwakyusa ameongeza kuwa, shirika litaendelea kutoa magari hayo kwa Halmashauri nyingine kwani wanatambua kuwa mahitaji bado ni makubwa kwa Mkoa wa Shinyanga, lakini pia wameanza na Wilaya ya Kahama kwa sababu ya idadi kubwa ya watu na eneo kuliko maeneo mengine Mkoani hapa.
Naye Mhe. Telack amewashukuru shirika la AGPAHI kwa magari hayo, lakini pia pamoja na wadau wengine wa sekta ya Afya kwa ushirikiano mkubwa na Serikali ya Mkoa kwa kazi kubwa wanayofanya na matokeo yake kiwango cha maambukizi ya UKIMWI kimeshuka kutoka 7.4 mwaka 2017 hadi 4.6 mwaka huu.
“Kazi mnayofanya ni kujenga familia za Watanzania hivyo muendelee kufanya kazi hiyo nzuri, Shinyanga kuna migodi mingi na kule wanakaa wananchi wengi hasa vijana, hivyo kupitia magari haya wataalamu wetu watafika na kutoa huduma huko”.
Amewataka Wakurugenzi wa Halmashauri za Kahama Mji na Ushetu kuhakikisha magari hayo yanakwenda kufanya kazi iliyokusudiwa.
Boma Street, Mwanza Road
Anuani: P.O.Box 320, Shinyanga
Simu: +255 28 2762222
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@shinyanga.go.tz
Hakimiliki@2018. Mkoa wa Shinyanga. Haki zote zimehifadhiwa