Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Zainab Telack amekemea kitendo cha baadhi ya viongozi kutumia madaraka yao vibaya kuwanyanyasa watumishi.
Akizungumza na viongozi pamoja na wananchi katika kata ya Songwa Wilayani Kishapu mapema leo katika ziara yake ya kukagua miradi ya afya na maji, Mhe. Telack ameonesha hisia zake za kukerwa na kitendo cha hivi karibuni cha mtumishi Afya kupigwa na Diwani akiwa kazini katika kituo cha Afya cha Bunambiyu Wilayani hapo.
Amesema siyo vizuri kuwavamia watumishi na kuwapiga na hataki kusikia suala hilo linajirudia katika Mkoa wa Shinyanga.
Amewata wananchi kutoa taarifa mahali panapohusika endapo wanaona hawapati huduma kwa kuanza na viongozi wa vijiji, Wilaya na hata Mkoa kuliko kutumia madaraka vibaya na kusababisha aibu katika Mkoa.
Tukio la kupigwa mtumishi limetokea hivi karibuni katika kata ya Bunambiyu, Wilayani Kishapu ambapo mtumishi wa kituo cha Afya cha kata hiyo bi. Hilda Simon alipigwa na Diwani baada ya kupigiwa simu na mgonjwa aliyedai hakupata huduma hali iliyosababisha taharuki kwa watumishi wa kituo hicho.
Naye Bi. Asha Bwanga ambaye ni mtumishi wa kituo cha Afya cha Songwa amesema tukio hilo liliwapa simanzi na taharuki watumishi wengine hivyo amemshukuru Mhe. Mkuu wa Mkoa kwa kukemea vitendo hivyo.
Boma Street, Mwanza Road
Anuani: P.O.Box 320, Shinyanga
Simu: +255 28 2762222
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@shinyanga.go.tz
Hakimiliki@2018. Mkoa wa Shinyanga. Haki zote zimehifadhiwa