Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Mboni Mhita, leo Septemba 15, 2025, amekutana na ujumbe kutoka Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi ofisini kwake, kwa lengo la kujadiliana kuhusu hatua za kuimarisha upatikanaji wa hati miliki na matumizi bora ya ardhi mkoani humo, hususan katika Wilaya ya Ushetu.
Katika kikao hicho, Naibu Kamishna wa Tume hiyo kwa Mkoa wa Shinyanga, Bw. Leo Komba, ameahidi kuwa zaidi ya hati 1,000 zitatolewa kwa wananchi wa Ushetu kama sehemu ya juhudi za Serikali kuimarisha usalama wa milki za ardhi na kupunguza migogoro.
Mhe. Mhita ameipongeza Tume hiyo kwa hatua wanazochukua katika kuhakikisha wananchi wananufaika na ardhi yao kwa mujibu wa sheria. Amesema changamoto ya umiliki holela wa ardhi ni moja ya vikwazo vya maendeleo, hivyo upatikanaji wa hati utasaidia sana kuleta suluhu ya kudumu.
"Kupitia zoezi hili, tunatarajia kuona mwamko mkubwa wa wananchi kushiriki na kupata haki yao halali ya kumiliki ardhi. Hii pia itawawezesha kuitumia ardhi yao kama dhamana ya mikopo na fursa nyingine za maendeleo," amesema Mhe. Mhita.
Kwa upande wake, Bw. Komba amesema kazi hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa Mpango wa Matumizi Bora ya Ardhi ulioidhinishwa na Serikali, unaolenga kuimarisha matumizi sahihi ya ardhi, kukuza kilimo, biashara na utulivu wa kijamii.
Zoezi hilo la utoaji wa hati linatarajiwa kuanza mara moja katika vijiji mbalimbali vya Ushetu, ambapo wananchi watahamasishwa kushiriki kikamilifu ili kuhakikisha kila mmoja anapata hati yake kihalali na kisheria.
OFISI YA MKUU WA MKOA, MKOA WA SHINYANGA, 04 MTAA WA BOMA
Anuani: P.O.Box 320, 37180,SHINYANGA, TANZANIA
Simu: +255 28 2762222
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@shinyanga.go.tz
Hakimiliki@2018. Mkoa wa Shinyanga. Haki zote zimehifadhiwa