Na. Paul Kasembo, SHY RS.
MKUU wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Anamringi Macha ametoa wito kwa wananchi wote kujitokeza, kujisajili ili waweze kushiriki vema katika tukio muhimu la mbio za Shycom Alumni Marathoni litakalofanyika tarehe 21 Septemba, 2024 huku lengo kuu likitajwa kuwa ni kuchangia fedha zitakazoboresha miundombinu ya Chuo cha Shycom.
Macha ameyasema haya leo tarehe 14 Septemba, 2024 ofisini kwake alipokuwa akizungumza na wanahabari kuhusu umuhimu wa tukio hili ambapo pamoja na mambo mengine lakini pia amesema mbio hizi zitawezesha kuimarisha uhusiano, kuboresha afya, kutambua na kujenga vipaji, kuchangia damu na kwamba takribani washiriki 1000 wanatajiwa katika tukio hili.
"Naomba kutoa wito kwa wananchi wote kujitokeza, kujiandikisha na kushiriki kikamilifu katika mbio hizi za hisani zilizopewa jina Shycom Alumni Marathoni ili tuweze kutimiza lengo la kuchangia fedha kwa ajili ya ukarabati wa miundombinu, kuimarisha umoja, uhusiano wetu, kuboresha afya zetu, kubainisha na kujenga vipaji kwa vijana wetu na kuchangia damu itakayowasaidia wagonjwa katika vituo vyetu vya afya," amesema Macha.
Aidha, Serikali ya Mkoa wa Shinyanga imewahakikishia usalama wakati wote wanamichezo wote watakaofika hapa mkoani Shinyanga na kushiriki katika Shycom Alumni Marathoni huku wafanyabiashara kutumia vema fursa ya uwepo wa mbio hizi kwani watu 1000 siyo wachache.
Shycom Alumni Marathoni ni mbio za hisani ambazo zimeandaliwa kwa maalum kwa waliosoma au kupita Shycom tangu kuanzishwa kwake wakiwemo waliokuwa Wadhibiti na Wakaguzi Wakuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kama vile Charles Kichere na ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Waziri wa Elimu Mhe. Adolf Mkenda (MB) sanjari na mwenyeji wake ambaye ni Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Macha.
Boma Street, Mwanza Road
Anuani: P.O.Box 320, Shinyanga
Simu: +255 28 2762222
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@shinyanga.go.tz
Hakimiliki@2018. Mkoa wa Shinyanga. Haki zote zimehifadhiwa