Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Mboni Mhita @mboni_mhita ametoa wito kwa viongozi wa dini, viongozi wa kimila na jamii kwa ujumla kuweka mikakati madhubuti ya kukomesha mmomonyoko wa maadili, hasa miongoni mwa watoto na vijana.
Akizungumza katika kikao kilichoratibiwa na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa kupitia Idara ya afya ustawi wa jamii na lishe kwa kushirikiana na shirika la ICS kilichofanyika leo Septemba 24, 2025 kwenye ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mhe. Mhita amesema mmomonyoko wa maadili umechukua kasi kubwa, huku athari zake zikijidhihirisha kwa familia kuvunjika, ongezeko la utoro mashuleni, watoto wa mitaani, na vitendo vya uhalifu.
“Leo hii tunaona familia zikivunjika, watoto wakitoroka mashuleni, wengine wakikimbilia mitaani na kujiingiza kwenye vitendo vya uhalifu. Haya yote ni matokeo ya mmomonyoko wa maadili ambao mizizi yake ni kulegalega kwa malezi katika ngazi ya familia,” alisema
Akitaja sababu kuu zinazopelekea hali hiyo, alieleza kuwa ni pamoja na Wazazi na walezi kushindwa kutimiza wajibu wao, Jamii kujitoa kwenye jukumu la pamoja la malezi, Kukosekana kwa hofu ya Mungu na kuiga mitindo ya maisha ya kigeni isiyoendana na maadili ya Kitanzania.
Aidha, Mhe. Mhita alisisitiza umuhimu wa kutekeleza kwa vitendo Programu Jumuishi ya Taifa ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto, akisema ni njia bora ya kuhakikisha watoto wenye umri wa miaka 0 hadi 8 wanalelewa katika mazingira yenye maadili, usalama na mwongozo wa kimaadili.
“Kama tutafanikiwa kuwalea watoto wetu vizuri kuanzia sasa, tutakuwa na vijana wenye maadili, wanaoheshimu wakubwa, wanaojitambua na wanaowajibika kwa jamii. Hili linawezekana iwapo kila mmoja wetu atachukua jukumu lake kwa uzito,” aliongeza.
Kikao hicho, kiliwashirikisha kamati ya maridhiano na amani mkoa, viongozi wa dini mbalimbali,viongozi toka makundi maalumu kama smaujata. Umoja wa wanaume, Baraza la Wazee Mkoa, vyama vya watu wenye ulemavu, Ofisi ya Magereza Mkoa, wataalumu toka ngazi ya Mkoa na Mdau kinara wa malezi ICS.
OFISI YA MKUU WA MKOA, MKOA WA SHINYANGA, 04 MTAA WA BOMA
Anuani: P.O.Box 37180,SHINYANGA, TANZANIA
Simu: +255 28 2762222
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@shinyanga.go.tz
Hakimiliki@2018. Mkoa wa Shinyanga. Haki zote zimehifadhiwa