Wananchi wa Mkoa wa Shinyanga wamehimizwa kujitokeza na kutoa ushirikiano kwa wataalamu wa utafiti wa viashiria na matokeo ya Virusi vya UKIMWI ili kupata mwelekeo wa hali ya ugonjwa huo hapa nchini.
Akizungumza wakati akifungua Mkutano wa kuutambulisha utafiti huo Mkoani hapa mwishoni mwa wiki, Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Zainab Telack amesema kuwa utafiti huu ni wa kipekee ambao kwa mara ya kwanza unahusisha wananchi wa rika zote.
Mhe. Telack amesema utafiti huu pia utaangalia kuwepo kwa viashiria vya usugu wa dawa, homa ya ini pamoja na ugonjwa wa Kaswende ambapo utakuwa na vipimo vingi zaidi ikilinganishwa na tafiti zilizopita.
Telack ametoa wito kwa wananchi wote wa Mkoa wa Shinyanga ambao watapitiwa kwa ajili ya kuhojiwa watoe ushirikiano ili kuweza kupata takwimu sahihi za hali ya ugonjwa wa UKIMWI kwa sasa kwani utafiti wa mwisho ulifanyika mwaka 2010/2011.
Awali akimkaribisha Mhe. Mkuu wa Mkoa kufungua Mkutano huo, Katibu Tawala wa Mkoa wa Shinyanga Bw. Albert Msovela amesema ni imani yake kuwa kupitia utafiti huu kutapatikana viashiria halisi na kupata takwimu ambazo ni sahihi zaidi kwani toka utafiti wa mara ya mwisho ulipofanyika ni muda mrefu sasa.
Utafiti huo unaofanywa na shirika la ICAP kwa kushirikiana na Ofisi ya Taifa ya Takwimu pamoja na Wizara ya Afya, Jinsia, Wazee na Watoto ulianza tangu mwezi Oktoba, 2016 na tayari umeshafanyika kwenye Mikoa 10 Tanzania.
Boma Street, Mwanza Road
Anuani: P.O.Box 320, Shinyanga
Simu: +255 28 2762222
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@shinyanga.go.tz
Hakimiliki@2018. Mkoa wa Shinyanga. Haki zote zimehifadhiwa